Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Binilith Mahenge (kushoto) na viongozi wengine wakikagua mradi wa maji wa Kintinku Lusilile uliopo Manyoni mkoani hapa wakati Kamati ya Siasa ya mkoa huo ilipo kuwa ikikagua miradi hiyo jana.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akipanda kukagua mradi wa maji wa Kintinku Lusilile uliopo wilayani Manyoni.
Muonekano wa tenki la maji mradi wa maji Kintinku Lusilile uliopo wilayani Manyoni.
Ukaguzi wa mradi wa maji Kintinku Lusilile uliopo wilayani Manyoni ukiendelea.
Ukaguzi wa madarasa Shule ya Msingi Heka ukiendelea.
Muonekano wa Vyoo vipya vilivyojengwa Shule ya Msingi Heka.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Heka Zamoyoni Mgumba akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa mawili.
Diwani wa Kata ya Heka, Haruna Thomas akizungumza wakati wa ukaguzi huo.
Ukaguzi wa mradi wa maji Kijiji cha Kitopeni Wilaya ya Itigi ukiendelea.
Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Manyoni Mhandisi Gabriel Ngongi akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi wa maji Kijiji cha Kitopeni uliopo Wilaya ya Itigi.
Taarifa ya ujenzi wa mradi wa maji Kijiji cha Kitopeni ikitolewa,
Ukaguzi wa madarasa yaliyojengwa Shule ya Sekondari ya Itigi ukiendelea.
Muonekano wa madarasa ya Shule ya Msingi Mlowa yaliyojengwa.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mlowa, Isaya Ntandu akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa mawili.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Singida Diana Chilolo akichangia jambo kwenye ukaguzi wa Kituo cha Afya cha Chibumagwa.
Ukaguzi wa moja ya jengo la kituo cha Afya Chibumagwa ukiendelea.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida, Davis Nyiraha akizungumza wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa madarasa mawili ya Shule ya Msingi Mlowa iliyopo Itigi.
Na Dotto Mwaibale, Singida
KAZI nzuri ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na Itigi imekonga nyoyo za wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida wakati walipokuwa wakikagua miradi hiyo.
Miradi hiyo imetekelezwa na halmashauri hizo kwa wakati baada ya kupatiwa fedha na Serikali ili kujenga miundombinu ya maji, ujenzi wa zahanati, miradi ya maji, madarasa na maabara.
Wajumbe hao wakizungumza kwa nyakati tofauti jana wakati wakikagua miradi hiyo walisema wameliridhishwa na utekelezaji wake licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo.
Akizungumzia miradi hiyo Mjumbe wa Kamati hiyo Diana Chilolo alisema kazi kubwa imefanyika katika kutekeleza miradi hiyo katika wilaya zote hizo mbili.
"Tumetembelea miradi mbalimbali na tumeridhishwa na utekelezaji wake na kujenga imani kwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ," alisema Chilolo..
Mjumbe wa kamati hiyo Yohana Msita alisema miradi mingi iliyotekelezwa imelingana na fedha halisi walizopewa na Serikali.
"Watekelezaji wa miradi hii wameonesha uaminifu mkubwa wa matumizi ya fedha walizopewa kwa ajili ya kuitekeleza," alisema Msita.
Martin Lissu mjumbe wa kamati hiyo alisema kasoro ndogo ndogo ambazo zimejitokeza wakati wa kujenga maabara katika baadhi ya shule za sekondari kama kuweka nondo kwenye madirisha na milango kufungukia ndani badala ya nje kwa ajili ya tahadhari ya majanga ya moto wametoa ushauri wa kuzirekebisha.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Alhaji Juma Kilimba alisema miradi hiyo inafanywa ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Kilimba alisema ameridhishwa na utekelezwaji wa miradi hiyo iliyofanywa katika halmashauri hizo.
"Kwa kweli tunawapongeza kwa kuitendea haki miradi hii ambayo Serikali inatumia fedha nyingi kuitekeleza," alisema Kilimba.
Kilimba alitumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi ilipo miradi hiyo kuwahamasisha wananchi wao kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii badala ya kuisubiri Serikali.
Alisema Serikali inafanya kazi kubwa ya kutoa fedha za miradi na ni wajibu wa wananchi nao kuhamasika kuunga jitihada za serikali kwa kujitolea kufanya kazi zingine za maendeleo ambazo zipo ndani ya uwezo wao.
Aidha Kilimba akizungumza kwa nyakati tofauti aliwataka wananchi na viongozi waliofika kushuhudia ukaguzi huo kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa corona.
Aliwaomba wananchi kila ilipotekelezwa miradi hiyo kuitunza ili iendelee kuwa na manufaa kwao.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge aliomba miradi ambayo bado haijakamilika ikamilike haraka ili wananchi waanze kunufaika nayo kwani imetumia fedha nyingi kutoka Serikalini.
Miradi iliyokaguliwa na kamati hiyo katika Wilaya ya Manyoni ni ujenzi wa madarasa mawili Shule ya Msingi Heka, ujenzi wa mradi wa maji Kintinku Lusilile, ukamilishaji wa maabara Shule ya Sekondari Mlewa, kutembelea mradi wa Kilimo cha umwagiliaji Kata ya Chikuyu na kuona changamoto ya mfumo wa maji kuacha njia badala ya kwenda kwenye mashamba yana elekea maeneo mengine kutokana na mafuriko na ujenzi wa Kituo cha Afya Chibumagwa.
Katika Wilaya ya Itigi miradi iliyotekelezwa ni ukamilishaji wa maabara na vyoo Shule ya Sekondari Itigi, ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa Shule ya Msingi Mlowa na ujenzi wa mradi wa maji wa Kijiji cha Kitopeni.
Ziara hiyo ya ukaguzi wa miradi hiyo iliwahusisha viongozi na wataalamu mbalimbali wa wilaya hizo.
Leo kamati hiyo itahitimisha ziara yake kwa kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
0 Comments