Serikali kwa kushirikiana na shirika la IMA World Health imezindua kampeni ya usawazishaji wa vikope kwa wananchi wenye matatizo ya macho kwenye wilaya za Sumbawanga na Kalambo mkoa wa Rukwa.
Uzinduzi wa kampeni hiyo unalenga kuwafikia wananchi zaidi ya Mia Sita (600) waliobainika kuwa na matatizo ya vikope (Trakoma) kufuatia utafiti uliofanywa na shirika la IMA World Health kwenye wilaya hizo ambapo huduma ya usawazishaji itafanyika kwa njia ya upasuaji mdogo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jana (18.08.2021) katika Kituo cha Afya Matai wilaya ya Kalambo, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryoba aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alisema lengo ni kuwatibu wote wenye matatizo ya macho ili waone vizuri.
“Kuwa na tatizo la vikope siyo dhambi, ni ugonjwa kama yalivyo magonjwa mengine hivyo nawasihi wote wenye shida hii kujitokeza kwenye kampeni hii ili kupata huduma ya matibabu inayotolewa bure na shirika la IMA World Health” alisema Waryoba.
Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kusema tatizo la vikope linatibika na kuwa wananchi hawana budi kujitokeza na kupata matibabu kwenye vituo vya afya ili wakipona waweze kuendelea kuona vizuri na kuendelea na maisha kawaida kwenye jamii.
Kwa upande wake Afisa Mratibu wa shirika la IMA World Health Dkt. William Hyera alisema mkoa wa Rukwa kufuatia utafiti umeonesha una wagonjwa zaidi ya 600 wenye matatizo ya vikope unaopelekea wasione vizuri hivyo kuhitaji matibabu.
“Kwa sasa wilaya ya Kalambo imekisiwa kuwa na wagonjwa 271 huku Sumbawanga ikiwa na wagonjwa 354 kwa hiyo kwa sasa tunatarajia kufanyia upasuaji kwa wagonjwa takribani 600 ingawa bado kuna wilaya zingine bado hatujapewa kibali hivyo hatuwezi kuzungumzia ”, alisema Dkt. Hyera.
Aliongeza kusema utambuzi wa wagonjwa unafanywa kwa ushirikiano na wataalam wa afya waliopatiwa mafunzo kwenye ngazi za vijiji na kata ili kuwezesha wafikiwe na huduma ambapo mwitikio ni mkubwa .
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu alisema ugonjwa wa vikope sasa ni moja ya magonjwa ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele kama kichocho, matende (mabusha) ambayo yanasababishwa na minyoo hivyo serikali imedhamiria kuyapatia matibabu.
Dkt. Kasululu aliongeza kusema ugonjwa unaoitwa vikope au Trakoma unaathiri eneo la kope za macho hasa za juu hatua inayopelekea kope zitazame ndani na hatua inayoweza kusababisha upofu usipotibiwa mapema.
“Wagonjwa wenye matatizo haya msijifiche ndani nendeni kwenye vituo vya afya kupata huduma ili kuepuka madhara ya upofu na kuwa huduma ya matibabu inatolewa bure “alisisitiza Dkt. Kasululu.
Awali akitoa taarifa ya mkoa, Dkt. Kasululu alisema takwimu za wagonjwa wa vikope kwa mkoa wa Rukwa waliokuwa wamejitokeza zinaonesha kwenye mabano kuwa mwaka 2018 (27), mwaka 2019 (50) na hadi Juni 2021 (73) lakini takwimu za utafiti zinasema wanaweza kuwepo zaidi ya 1,000.
Kampeni hii yenye kauli mbiu “Epuka Upofu, Wahi Matibabu ya Kusawazisha Kope”itakamilika ifikapo mwezi Aprili mwaka 2022 kwa mkoa wa Rukwa.
Mwisho.
Imeandaliwa na;
Afisa Habari Mkuu,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,
SUMBAWANGA
18.08.2021
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryoba akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwenye uzinduzi wa kampeni ya usawazishaji wa Vikope kwa wananchi wenye matatizo ya macho jana kwenye Kituo cha Afya Matai wilaya ya Kalambo.(Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa)
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Tano Mwera akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya Tokomeza Vikope jana kwenye uzinduzi uliofanyika kijiji cha Matai wilayani humo ambapo amewataka wote wenye matatizo ya macho kwenda kwenye vituo vya afya kupata tiba ili kuepuka upofu.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu (aliyesimama) akizungumza kuhusu umuhimu wa kampeni ya Tokomeza Vikope jana wilayani Kalambo unaofanywa na serikali kwa kushirikiana na shirika la IMA World Health. Kushoto wa kwanza ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastin Waryoba akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Tano Mwera.
0 Comments