Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT.MABOKO AUPONGEZA MKOA WA MTWARA WALIVYOJIPANGA KATIKA KUPAMBANA NA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU


Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko alipotemebelea ofisini kwake kwa lengo la kufahamiana na uongozi wa mkoa pamoja na kufatilia utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI katika mkoa huo

****************************

Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania imeridhishwa na utekelezaji wa shughuli za mwitikio wa UKIMWI zilizotekelezwa Mkoani Mtwara katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI mratibu wa UKIMWI mkoa wa Mtwara Bi Tabitha Kilangi amesema kwamba, kiwango cha maambukizi kimeendelea kushuka kutoka silimia 4.1 kwa utafiti wa viashiria vya UKIMWI vya mwaka 2011/12 hadi asilimia 2.0 kwa utafiti wa mwaka 2016/2017.

Ameongeza kuwa, watu wanaoishi na VVU wanafahamu hali zao za maambukizi kwa asilimia 82 na watu waliopo kwenye utaratibu wa kutumia dawa za kufubaza VVU (ARV) hadi kufikia Januari, 2021 ilikua ni asilimia 92. Watumiaji wa dawa hizo wameweza kupunguza kiwango cha VVU kwenye miili yao kwa asilimia 94.

Aidha ameainisha njia zinazotumika katika mkoa huo ni pamoja na kusisitiza upimaji wa hiari, kuendesha kampeni na ushawishi, kutoa elimu kupitia redio za kijamii, mikutano ya hadhara, vikundi vya Sanaa, vipeperushi, majarida na mabango, kutoa huduma za VVU na UKIMWI majumbani, kutoa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kama vile sare za shule ,vifaa vya shule ada ana matibabu. utoaji wa elimu kuhusu matumizi sahihi na endelevu ya kondomu na kutambua makundi maalum kama wafanyabishara ya ngono na kupanga mikakati ya kuzuia maambukizi mapya.

Aidha amesema pia serikali inashirikiana kwa karibu na wadau wa nje na wa ndani katika kupambana na maambukizi ya VVU ambapo katika mwaka 2020/2021 mkoa kwa kushirikiana na halimashuri na wadau mbalimbali uliweza kuchangia sh. 254,086,963 kwa ajili ya utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI.

Naye kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bwana Renatus Mongogwela amesema kwamba, kwa kushirikana na wadau bado kuna umuhimu wa kusisitizia matumizi sahihi na endelevu ya kondomu, ili wananchi wasione aibu kwenda dukani kununua kondomu kutokana na umuhimu wake.

“kwa sasa suala la matumizi ya kondomu bado lina unyanyapaa sana kwa kuwa mtu akikuona una nunua kondomu lazima akushangae, kumbe kwa sasa kondomu ni bidhaa kama bidhaa nyingine, kwa kuwa ni kwa faida yetu binafsi. Nawasihi watanzania tusinyanyapaane kwa kuwa kondomu inasaidia mambo mengi sana mbali na kukinga maambukizi ya VVU lakini pia inakinga mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya ngono” amesema Mongogwela.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt Leonard Maboko ameupongeza uongozi wa mkoa huo jinsi walivyojipanga katika kupambana na maambukizi mapya ya VVU.

Amesema kama kila Mkoa utajipanga na kufanya kazi hivi basi ifikapo 2030 tutaweza kufikia malengo yatu ya Tanzania bila UKIMWI inawezekana, suala la kushirikiana na wadau ni la muhimu sana kwakuwa sasa hivi ni muhimu tujipange kutumia raslimali zetu za ndani katika mapambano ya VVU.

Dkt Maboko alitembelea Mkoa wa Mtwara kwa lengo la kufanya ufuatiliaji na Tathimini ya afua za VVU na UKIMWI zinazotekelezwa katika mkoa huo.

Post a Comment

0 Comments