Serikali imewataka wanachama wa chama cha waganga na wakunga wa tiba asili na mbadala Mkoa wa Rukwa (CHAWATIRU) kujisajili na kusajili dawa zao kwenye Baraza la Taifa la Tiba Mbadala ili wawe huru kutoa huduma kwa jamii.
Wito huo umetolewa leo (09.08.2021) Sumbawanga na Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Asili na Tiba Mbadala toka Wizara ya Afya Dkt. Paulo Mhame wakati wa kikao kazi na wanachama wa Chawatiru kwa lengo la kuwaelimisha shughuli zao ili kukabiliana na tatizo la UVIKO-19.
"Wito wa serikali ni kuona watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala wote wanasajiliwa na dawa zao zinatambuliwa na Mkemia Mkuu wa Serikali ili muwe huru kutoa huduma za tiba na kuwezesha maisha ya watu kuwa salama " alisema Dkt. Mhame
Faida za dawa za tiba asili kusajiliwa na kupimwa ni kuwezesha kutambua usalama wake na kuwezesha kukuza soko la dawa ndani na nje ya nchi alisema Mkurugenzi huyo aliyebobea kwenye tiba asili.
Dkt. Mhame aliongeza kusema tiba asili ilitoa mchango mkubwa kwenye kukabiliana na janga la UVIKO-19 wimbi la kwanza pale ambapo serikali na wadau wa kimataifa walikuwa hawajapata kinga, hivyo njia asili za kujiepusha na kifo ikiwemo kujifukiza ilitumika na kuwa na matokeo mazuri.
Kwa kuwa chanjo sasa imepatikana serikali inawaelimisha watu wapate chanjo hiyo kutokana na uwezo wake wa kusaidia kupunguza maambukizi ya UVIKO-19 na kuongeza kuwa " mtu ambaye si mgonjwa anahitaji kinga ndio maana sasa serikali inatoa chanjo. Lengo letu hatutaki mtu argue kabisa Corona" alisisitiza Dkt. Mhame.
Katika hatua nyingine Dkt.Mhame amewaonya waganga wa tiba asili kujiepusha na uvunjifu wa sheria ikiwemo vitendo vya mauaji, ubakakaji na vitendo vya kuharibu nyara za serikali kwa kigezo cha kutaka kutambulika kwenye jamii.
"Kutokuwa na ngozi ya Simba au kucha zake hakukufanyi usiwe mganga wa tiba asili maarufu. Muhimu tambua sheria na taratibu za huduma za tiba mbadala na tiba asili . Hii ni huduma muhimu kwa jamii" alisema Dkt. Mhame.
Mkurugenzi hyuo ya Idara ya Tiba Asili na tiba mbadala aliwaeleza waganga hao wa tiba asili kutoka wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo kuwa Wizara ya Afya inahamasisha watanzania katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Corona ni budi wakapata chanjo ili kujikinga na virusi vya UVIKO-19 wao pamoja wateja wao.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu alisema mkoa wake una waganga wengi wa tib asili ambao wanatoa huduma kwa jamii hivyo kikao kazi hicho kimelenga kuwatambua na kujadiliana namna bora ya kufanikisha utoaji huduma kwa uwazi na ubora kipindi hiki cha kupambana na UVIKO-19
Dkt. Kasululu alibainisha kuwa huduma za tiba asili zipo tangu enzi za mababu na zinaaminiwa na wananchi na kuwa zipo kwa mujibu wa sheria na taratibu hivyo waganga hao lazima watekeleze kazi zao kwa uwazi ikiwemo kujisajili kwenye Baraza la Tiba asili nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama chanWaganga na Wakunga qa Tiba Asili na Tiba Mbadala mkoa wa Rukwa ( CHAWATIRU) Timothy Brucks alishukuru serikali kupitia ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuwakutanisha hatua inayokuwa maelewano baina ya wataalam wa serikali na waganga wa tiba asili .
Timothy alisema kikao hicho kimesaidia kuongeza uelewa na majukumu ya waganga wa tiba asili na tiba mbadala kwenye kupambana na UVIKO-19 hatua itakayosaidia jamii ya watanzania kuwa salama.
Mwisho.
Imeandaliwa na
Revocatus Kassimba,
Afisa Habari Mkuu,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
Sumbawanga
09.08.2021
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu (katikati) akizungumza na Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala leo kuhusu umuhimu wa kujisajili na kusajili dawa zao ili wawe huru kutoa huduma kwa jamii.
Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Asili na Tiba Mbadala Wizara ya Afya Dkt. Paulo Mhame akizungumza na wanachama wa chama cha waganga wa tiba asili na tiba mbadala mkoa wa Rukwa (CHAWATIRU) leo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa kuhusu mchango wa tiba asili kwenye kukabiliana na UVIKO-19. Kulia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu.
Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Asili na Tiba Mbadala Wizara ya Afya Dkt.Paulo Mhame akizungumza na wanachama wa chama cha waganga wa tiba asili na tiba mbadala mkoa wa Rukwa (CHAWATIRU) leo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa kuhusu mchango wa tiba asili kwenye kukabiliana na UVIKO-19. Katikati ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu.
0 Comments