Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Khamis Hamza Chilo akizungumzia Hatua ya Serikali kupeleka Chanjo ya UVIKO-19 katika makazi na makambi mbalimbali ya wakimbizi yaliyopo nchini wakati alipofanya ziara ya kikazi leo katika Kituo cha Afya cha Katumba mkoani Katavi.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
*************************
Na Abubakari Akida,MOHA
Serikali imesema iko katika mpango wa kupeleka Chanjo ya UVIKO 19 katika Makambi na Makazi ya Wakimbizi katika mikoa ya Kigoma,Tabora na Katavi ikiwa ni mpango mkakati wa kukabiliana na wimbi la tatu la ugonjwa huo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Khamis Hamza Chilo wakati alipotembelea Kituo cha Afya cha Katumba kinachotumiwa na wakimbizi na raia wapya wanaokadiriwa kufikia 86,233 toka nchini Burundi ambao walikimbia mapigano ya kikabila yaliyotokea nchini kwao 1974.
“Katika kukabiliana na janga la UVIKO 19 tayari Wakuu wa Makambi washaanza kutambua idadi ya watu ambao wanauhitaji wa hiari wa kupata chanjo hiyo ili jamii ya wakimbizi wanaokaa katika makambi yaliyopo nchini ili muda ukifika tuwe na takwimu sahihi za wanaohitaji kuchanjwa na tayari kama mnavyoona tayari zoezi la chanjo lishaanza baada ya siku chache kuzinduliwa na Rais Mama Samia Suluhu Hassan na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu,wito pekee naotoa kwa wakimbizi kufuata ushauri wa wataalamu wa afya katika kujikinga na maradhi hayo ambayo dunia sasa inapitia” amesema Naibu Waziri Chilo
Akizungumzia idadi ya wagonjwa wa UVIKO 19 katika Kituo cha Afya Katumba, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho,Dkt.Veneranda Msati amesema hawana mgonjwa aliyefika kituoni huku akielezea utolewaji wa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo kwa wagonjwa na mama wajawazito wanaofika katika kituo hicho kupata huduma.
“Kwasasa katika kituo chetu hatuna mgonjwa yoyote wa Corona tunachofanya ni kutoa ushauri wa kujikinga na maradhi hayo kwa wagonjwa wanaofika hapa kupata huduma za afya ikiwemo na akina mama wajawazito lakini pia tunatuma wataalamu wetu wa afya kwenda kuwafundisha wananchi katika makazi yao jinsi ya kunawa kwa maji safi tiririka na kukaa umbali unaoshauriwa ili kuepuka maambukizi ya UVIKO”amesema Dkt. Veneranda
Awali akisoma taarifa ya makazi hayo,Mkuu wa Makazi ya Katumba,John Mwita amesema hali ya usalama ni shwari huku wakiendelea kutoa elimu na kufuata sheria za kuishi katika makazi kwa wakimbizi hao.
0 Comments