Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid
Tamatamah akizungumza wakati wa ziara hiyo kushoto ni Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Mashimba Ndaki akifuatiwa na Mkuu wa wilaya ya Pangani |
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki kulia akikagua jengo la BMU Kijiji
cha Zingibar wilayani Mkinga wakati wa ziara yake kushoto ni Mbunge wa
Jimbo la Mkinga (CCM) Dastan Kitandula |
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki kushoto akiwa na Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah wakikagua jengo la BMU Kijiji cha Zingibar wilayani Mkinga wakati wa ziara hiyo |
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki akiendelea na ukaguzi wa Jengo la BMU Kijiji cha Zingibar |
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki kushoto akikagua Jengo la BMU Kijiji cha Zingibar wilayani Mkinga wakati wa ziara yake kulia ni Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki kushoto akigawa vifaa vyenye thamani ya Shilingi Milioni Nne kwa ajili ya kilimo cha mwani kwa vikundi vitatu vya wakulima wa zao hilo wilayani Mkinga |
NA OSCAR ASSENGA, PANGANI.
SERIKALI
inatarajiwa kutumia Shilingi Bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa soko la
kimataifa la kuuzia dagaa Kata ya Kipumbwi Wilaya ya Pangani Mkoani
Tanga ambalo litatumika na wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki wakati wa ziara
yake ya kikazi ya siku moja mkoani humo, iliyoambatana na ukaguzi wa
majengo ya Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika
Wilaya za Mkinga na Pangani.
Majengo hayo yaliyojengwa kupitia mradi wa Usimamizi
Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi
(SWIOFISH).
Alisema
wanunuzi wa dagaa wanaotoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,
Zambia, Malawi, Rwanda na Burundi wataenda kununua dagaa kutoka Kipumbwi
hivyo wafanyabiashara wa kata hiyo hawatapata shida ya kutafuta soko la
dagaa.
“Niwaambie
serikali imesikia na inakusudia kujenga kujenga soko la Kimataifa la
kuuza dagaa, msipate shida kuuza dagaa wenu.” Alisema
Waziri Ndaki.
Aidha, Waziri Ndaki alitoa onyo kwa viongozi wa BMU maeneo mbalimbali
nchini, ambao wamekuwa wakishiriki vitendo vya uvuvi haramu pamoja na
baadhi ya wavuvi kuwa vikundi hivyo vitavunjwa na wahusika kuchukuliwa
hatua kali za kisheria.
Alifafanua
pia baadhi ya BMU zimekuwa zikishindwa kutekeleza wajibu wake na
kujikuta wakishirikiana na wavuvi haramu ambapo aliwataka kuacha vitendo hivyo kabla hawajakumbana na mkono wa sheria.
Akiwa
wilayani Mkinga kwenye Kijiji cha Zingibari, Waziri Ndaki alisema
serikali itaendelea kuwawezesha wakulima wa mwani kwa vifaa pamoja na
utaalamu ili waweze kuzalisha kwa tija zao hilo kwa wingi na ubora
unaohitajika sokoni.
Alitoa
kauli hiyo wakati akitoa vifaa vyenye thamani ya Shilingi Milioni Nne
kwa ajili ya kilimo cha mwani kwa vikundi vitatu vya wakulima wa zao
hilo wilayani Mkinga.
Alisema kuwa kutokana na zao hilo kuwa la kiuchumi kwa wananchi wa mwambao
wa pwani ya Bahari ya Hindi, serikali imeanza kuweka mazingira mazuri
ya uwezeshaji na kutafuta masoko ya uhakika ili wakulima
waweze kunufaika kiuchumi.
"Huu
msaada wa vifaa kwa ajili ya kilimo utafika katika maeneo yote yenye
uzalishaji na msisitizo tumeanza kuweka kwenye elimu ya
namna ya kulima zao la mwani kwa ajili ya tija zaidi." alisema Waziri Ndaki
Kuhusu
sekta ya mifugo, Waziri Ndaki alieleza sababu za kuanzishwa minada
kwenye mipaka mbalimbali hapa nchini ambapo ikiwa na lengo la
kuhakikisha wafugaji kutoka Tanzania wanauza mifugo kwenye minada hiyo
na wanunuzi wanatoka nchi nyingine kwenda kununua ili kudhibiti
utoroshaji.
Waziri
Ndaki alisema hayo baada ya kufika katika mnada wa mipakani wa Horohoro
kujionea miundombinu mbaimbali inayowekwa kabla ya kuanza rasmi kwa
mnada huo ambao anasema utakuwa na matokeo chanya pindi utakapokamilika.
“Licha
ya kusaidia kupunguza utoroshaji wa mifugo mnada utasaidia kuongeza
kipato kwa wananchi na hivyo kuinua uchumi wao, kwa sababu wakipeleka
ng’ombe nje ya nchi wanauza bei ya juu lakini pia tunataka tuwapunguzie
wananchi adha ya kuvuka mipaka kwani jambo hili wakati mwingine
linasababisha kuuza mifugo yao kwa bei ya
chini” Alisema
Hata
hivyo Waziri Ndaki alisema wameamua kuondoa shida hizo kwa kuwa na
minada ya mipakani ili wafugaji waweze kuuza mifugo yao maeneo rasmi na
serikali iweze kupata mapato yao .
0 Comments