NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Hifadhi ya misitu Asili maarufu kama The Amani Nature Reserve imezindua kampeni ya Unlock Amani inayolenga kutangaza utalii wa misitu asili na kutunza vyanzo vya maji ili kuhakikisha misitu endelevu na upatikanaji wa maji.
Kampeni hiyo ni safari maalumu ya siku tatu ambayo ni wazi kwa watu wote kwenda kuzuru Amani na kwenda kujionea vivutio vilivyopo na pia kufahamu mikakati iliyowekwa hadi sasa, safari hiyo imepangwa kufanyika kuanzia Agosti 27 hadi Agost 29, 2021.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Mhifadhi wa Amani Nature Reserve Bw.Bob Matunda amesema kampeni hiyo inalenga kutumia juhudi za pamoja kuhakikisha hifadhi hiyo inafahamika zaidi na jamii zinazoizingira kufahamu majukumu yao katika matumizi endelevu ya ardhi.
"Tunataka kuhakikisha kuwa tunafanya kazi kwa karibu na Serikali na wadau wengine katika kutunza vyanzo vya mto Zigi na Ruvu na kuhakikisha Mji wa Tanga unakuwa na maji ya kutosha muda wote". Amesema Bw.Matunda.
Aidha ameipongeza Wizara ya Maji kwa kupitia Mamlaka ya Pangani Water Basin, Mamlaka ya Misitu Tanzania, Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa na Vodacom kwa kuungana katika suala hilo la utunzaji wa vyanzo vya maji na misitu asili na tayari mafanikio yameanza kuonekana.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Kunusuru Vyanzo vya Maji Bonde la Wami Ruvu na Bonde la Pangani Bw.Bakari Bamba amesema ili kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali, ANR ilibuni vyanzo vingine vya kipato kama vile utalii wa misitu asili, ufugaji nyuki, samaki, vipepeo,matunda na mauana kilimo cha viungo ikiwemo pia kutafuta masoko ya mazao yanayopatikana na upatikanaji wa miche.
"Suala kama hili linahitaji ushirikiano wa hali ya juu kati ya taasisi za Serikali, Sekta binafsi na mashirika yasiyo ya Kiserikali ili kuhakikisha ardhi inatumika vizuri, maji yanapatikana kwa uhakika na wananchi wanakuwa na maisha bora zaidi". Amesema Bw.Bamba.
Nae Mtaalamu wa Miradi (UNDP) Bw.Abbas Kitogo amesema utunzaji wa vyanzo vya maji na misitu ni miongoni mwa vipaumbele vyao na wataendelea kuunga mkono jitihada hizo.
"Tunaamini katika mazingira na tunatoa wito kwa wadau wengine wajitokeze kujionea vivutio vilivyopo Amani Nature Reserve ". Amesema.
Hifadhi ya misitu asilia ya Amani imesema vyanzo vya maji na misitu asilia ni miongoni mwa vitu ambavyo vipo hatarini kuharibiwa na zinahitajika jitihada za pamoja
Mhifadhi wa Amani Nature Reserve Bw.Bob Matunda akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya Unlock Amani inayolenga kutangaza utalii wa misitu asili na kutunza vyanzo vya maji ili kuhakikisha misitu endelevu na upatikanaji wa maji iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Mbatilo)
Mratibu wa Mradi wa Kunusuru Vyanzo vya Maji Bonde la Wami Ruvu na Bonde la Pangani Bw.Bakari Bamba akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya Unlock Amani inayolenga kutangaza utalii wa misitu asili na kutunza vyanzo vya maji ili kuhakikisha misitu endelevu na upatikanaji wa maji iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Mbatilo)
Mtaalamu wa Miradi (UNDP) Bw.Abbas Kitogo akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya Unlock Amani inayolenga kutangaza utalii wa misitu asili na kutunza vyanzo vya maji ili kuhakikisha misitu endelevu na upatikanaji wa maji iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Mbatilo)
0 Comments