Ticker

6/recent/ticker-posts

WFC KUPUNGUZA KIWANGO CHA TOZO KUTOKA ASILIMIA  MOJA HADI 0.6 KWA WAAJIRI WA SEKTA BINAFSI

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), umetangaza rasmi kupunguza kiwango cha tozo kwa waajiri wa sekta binafsi kutoka asilimia moja hadi 0.6 kuanzia michango ya Julai mwaka huu, ikiwa ni punguzo la asilimia 40, ili kuboresha mazingira ya biashara.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa WCF, Dkt. John Mduma, amesema marekebisho hayo yanafuatia uamuzi wa Bunge ambalo lilipitisha kiwango hicho cha tozo kwa sekta binafsi.

“Dhamira ya hatua hii ni kuzifanya sekta binafsi kutumia masalio ya fedha hizo katika uzalishaji, hivyo tumewapunguzia mzigo ili kukuza biashara zao". Amesema Dkt.Mduma.

Ameweka wazi kuwa hatua hiyo inaboresha mazingira ya biashara kama inavyoelekeza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuhusu kuziboresha taasisi kwa kuzipunguzia tozo.

Ameongeza pia hatua hiyo inalenga kuleta mahusiano mazuri kati ya mfuko huo na waajiri, hatimaye kuchangia ukuaji uchumi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, pamoja na kupunguza kiwango cha michango kwa sekta binafsi, lakini mafao yanabaki kama yalivyokuwa awali.

“Mchakato huu umepitia sehemu nyingi ninawashukuru Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) ambao wote kwa pamoja tumeshirikiana kufikia hatua hii,” amesisitiza.

Dkt. Mduma ameeleza kuwa kwa sasa mfuko huo una thamani ya sh. bilioni 437 na kwamba kumekuwa na kasi kubwa ya ongezeko la wachangiaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uendeshaji wa WCF, Bw. Anselim Peter, amesema mfuko huo una jumla ya wachangiaji 24,952 na kati yao sekta binafsi ni asilimia 70 huku 30 ni sekta ya umma.

Amebainisha kuwa pamoja na kupunguza asilimia ya michango, lakini tathmini zinaonyesha WCF itakuwa na afya kwa zaidi ya miaka 30 kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Amesema hadi sasa tayari wameshabadilisha mifumo yao ya kielektroniki, hivyo yeyote atakayelipa atatumia kikokotoo kipya cha asilimia 0.6.

Kuhusu idadi ya wachangiaji wanaozingatia michango hiyo, Peter amesema ni asilimia 82 huku waliobaki ndiyo changamoto.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar, amesema kiwango cha michango kwa sekta ya umma ni asilimia 0.5 huku sekta binafsi ni asilimia 0.6.

Amesema sababu za tofauti ya michango hiyo ni hali hatarishi zaidi kwa wafanyakazi wa sekta binafsi ukilinganisha na sekta ya umma kutokana na shughuli zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Francis Nanai, aliwahi kueleza kuwa, hatua hiyo ya kupunguzwa kwa kiwango hicho cha michango kutoka asilimia moja hadi 0.6, kitawawezesha kutanua wigo wa biashara zao.

Alisema iwapo biashara zitatanuka maana yake watakuwa na uwezo zaidi wa kuchangia mfuko huo, hivyo utatuna na kuwanufaisha wahanga.

Nanai aliongeza kuwa punguzo hilo sio tu litaongeza wachangiaji wa mfuko huo, bali litaiimarisha sekta binafsi na hivyo kuwa na mchango chanya katika uchumi wa nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za WCF leo Jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma (katikati) akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za WCF leo Jijini Dar es Salaam. kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar na kushoto ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa WCF, Bw. Anselim Peter.Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za WCF leo Jijini Dar es Salaam  Mkurugenzi wa Uendeshaji wa WCF, Bw. Anselim Peter akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za WCF leo Jijini Dar es Salaam.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

Post a Comment

0 Comments