-Aimwagia sita asasi ya Tayoa kwa ubunifu
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imeshauri Shirika la Vijana Tanzania (Tayoa) kusambaza makasha ya kusambazia mipira ya kinga (kondom) na ATM za mipira hiyo kwenye halmashauri zote 184 nchini kama sehemu ya kuchochea mapambano dhidi ya Ukimwi.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, wakati wa uzinduzi wa makasha ya kusambazia kondom aina ya safari zinazosambazwa na Tayoa sehemu mbalimbali nchini kupitia kampuni yake ya Vijanatz Industries Ltd .
Alisema watu wengi wanaona haya kwenda kununua mipira hiyo madukani kwa hofu kuwa wataonekana wahuni hivyo ubunifu wa Tayoa utasiadia watu wengi kuwa na faragha ya kwenda kununua kinga hiyo wanapotaka kufanya mapenzi.
Alisema angependa kuona makasha hayo na ATM hizo zinasambazwa maeneo yote nchini ili watu wajihudumie wenyewe kwani kwa sasa baadhi ya watu wanashindwa kwenda kuzinunu madukani kwa hofu ya kuonekana wahuni.
“Nawapongeza Tayoa huu ni ubunifu mkubwa saba kwasababu itasaidia sana watu wengi wanunue kondom na imekuwa mbaya sana hasa kwa wasichana kwasababu wakinunua mipira hii ya kinga wanaonekana malaya, mimi nawashauri wakina dada kwamba mkishindwa kujizuia kabisa kufanya ngono ni heri kuwa na kinga kuepuka mambo mengine,” alisema Ummy
Ummy alisema shirika hilo ambalo mwakani linatimiza miaka 24 halijawahi kupoteza mwelekeo wa malengo yao tangu kuanzishwa kwake kwani siku zote wamekuwa wakisimamia kupambana na ugonjwa wa Ukimwi ambao alisema bado upon a unaua watu wengi hapa nchini.
“Tayoa nawajua na tumefanyakazi nanyinyi hata kabla sijawa Naibu Waziri na baadaye Waziri, kwa muda wote niliowafahamu nyinyi mwelekeo wenu ni kupambana na ugonjwa wa Ukimwi hivyo nawapongeza kwa msimamo wenu thabiti wa kupambana na janga hili,” alisema Ummy.
Waziri Ummy aliwaomba viongozi wa serikali kwenye ngazi zote kuipa ushirikiano taasisi hiyo itakapokuwa inasambaza mipira hiyo na kuhakikisha makasha na ATM za mipira hiyo zinatunzwa kwaajili ya matumizi ya muda mrefu kwenye maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tayoa, Peter Masika alisema hadi sasa wameshasambaza makasha 40,000 katika Wilaya 169 nchini na kwamba wanatarajia kusambaza mengine 40,000 kwenye maeneo mbalimbali nchini hivyo kufikisha 80,000.
Alisema wanatarajia kuanza kusambaza mashine 5,000 za kutolea mipira hiyo (ATM) katika miaka miwili ijayo na kwamba makasha watakayosambaza yana pande mbili na yatasambazwa kwenye wilaya zote za Tanzania Bara.
Masika aliwashukuru wafadhili wa shirika hilo ambao ni Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi (Global Fund), Wizara ya Afya, Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto, Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) na Wizara ya TAMISEMI.
Alisema kwa sasa Tayoa kwa kushirikiana na AMREF wanatekeleza mradi wa Global Fund unaowalenga wasichana walio katika umri wa kubalehe na wanawake vijana katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Tanga, Singida na Geita kwani kundi hilo ndilo lililo katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu akionyesha kondom aina ya safari mara baaa ya kuitoa kwenye mashine ya kuuzia kondom kwa bei nafuu wakati wa uzinduzi wa makasha ya kondom mjini Dodoma jana. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Tayoa, Peter Masika ambaye alisema wanatarajia kusambaza makasha 80,000 nchini.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu akiwasili kwenye uzinduzi wa makasha ya kondom mjini Dodoma jana. Kulia kabisa Mkurugenzi Mkuu wa Tayoa, Peter Masika ambaye alisema wanatarajia kusambaza makasha 80,000 nchini. Mwingine ni Mbunge wa Dodoma Mjini Antony Mavunde
Vijana wa kikundi cha ngoma cha mjini Dodoma wakitumbuiza kwenye uzinduzi wa makasha ya kusambazia kondom mjini Dodoma uliofanywa na Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu ambapo shirika la vijana Tayoa linatarajia kusambaza makasha 40,000 nchi nzima.
Mkurugenzi Mkuu wa Tayoa Peter Masika akimfafanulia jambo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu namna makasha ya kusambazia kondom yanavyofanyakazi, mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa makasha hayo jijini Dodoma.
Read more
0 Comments