Na. James K. Mwanamyoto-Pwani
Tarehe
27 Julai, 2021
Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
amewataka Watumishi wa Umma nchini kulipa deni kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzani, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na kutumia
weledi wao kujenga uchumi wa taifa.
Akizungumza kwa nyakati
tofauti na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Halmashauri ya Wilaya ya
Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, Mhe. Ndejembi amesema
kuwa Mhe. Rais alipoingia madarakani, alitoa maelekezo kwa Waajiri wote kuzingatia
maslahi ya watumishi wa umma hususani suala la upandishwaji wa madaraja jambo ambalo
hivi sasa limetekelezwa na linaendelea kutekelezwa na waajiri wote kikamilifu ikiwa
ni pamoja na kulipa stahili za watumishi kwa wakati.
Amesema waajiri wote
nchini wametekeleza maelekezo ya Mhe. Rais, hivyo Watumishi wa Umma hawana budi
kufanya kazi kwa bidii na uadilifu kwani hakuna haki isiyokuwa na wajibu.
“Ni muda mrefu tumekuwa
tukililia haki ya kupandishwa madaraja na kupewa stahili nyingine, Rais wetu
ametusikia kwani wote waliostahili kupanda madaraja, wamepanda na wenye madai
ya stahili zao mbalimbali wamepatiwa, hivyo hili ni deni na ili kulilipa deni
hili tunapaswa kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu,” Mhe. Ndejembi
amesisitiza.
Ameongeza kuwa,
Serikali itaendelea kujali maslahi ya Watumishi wa Umma kwasababu watumishi
ndio injini ya Serikali, hivyo wanalazimika kuendelea kutekeleza wajibu wao
ipasavyo.
Aidha, Mhe. Ndejembi
amezungumzia changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika zoezi la upandishwaji
wa madaraja kwa Watumishi wa Umma kutokana na baadhi yao kukosa sifa kwa kutojaza
Fomu ya Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS).
“Changamoto ya
upandishwaji madaraja kwa baadhi ya Watumishi ni kupuuza ujazaji wa OPRAS,
hawajazi kwa wakati na wanajaza kwasababu wanaona ni kigezo tu cha upandaji wa
madaraja.” Mhe. Ndejembi amefanua.
Ili kuongeza ufanisi
kiutendaji, Mhe. Ndejembi amewahimiza Watumishi wa umma nchini kufanya kazi kwa
ushirikiano ili kufanikisha lengo la Serikali la kutoa huduma bora kwa
wananchi.
Katika hatua nyingine
Mhe. Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma kushiriki katika kutoa elimu kwa
walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanaonufaika na Mradi wa kutoa
ajira za muda.
Amesema suala la
usimamizi wa walengwa wa TASAF ni la watumishi wote, hivyo ni vema watumishi
wenye utalaam katika fani mbalimbali wakatoa elimu ya kuwawezesha walengwa kutimiza
malengo yao badala ya kuwaachia Waratibu wa TASAF pekee.
Aidha, amewataka
walengwa wa TASAF kutumia vizuri ruzuku wanayoipata kujikwamua katika lindi la
umaskini ili hapo baadae waache kutegemea ruzuku ya TASAF.
Kwa
upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Mhe. Ridhiwan Kikwete amesema kilio
kikubwa cha Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kilikuwa ni suala la
upandishwaji wa madaraja jambo ambalo limetekelezwa na Serikali ya Awamu ya
Sita.
“Mhe.
Naibu Waziri tunashukuru sana kwa kututembelea, changamoto kubwa iliyokuwa ikitusumbua
ni upandishwaji wa madaraja, suala ambalo limeshafanyiwa kazi, tunamshukuru
Mhe. Rais kwa kuliona hili na kulitekeleza.” Mhe. Ridhiwan ameongeza.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo.
Baadhi ya Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Afisa Misitu wa Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani, Bw. William Msemo akiwasilisha hoja ya kiutumishi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mji huo wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini wa Kitongoji cha Mwanabwito, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF mkoani Pwani.
Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi alipofanya ziara ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma Wilayani Chalinze.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Mhe. Michael Mwakamo akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi alipofanya ziara ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua miradi ya TASAF wilayani Kibaha.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TASAF, Bw. Paul Kijazi akitoa maelezo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuhusu mradi wa jengo la kitega uchumi la kikundi cha Wazee wa Mlandizi lililojengwa na TASAF.
Kikundi cha Wazee wa Mlandizi kilichonufaika na mradi wa jengo la kitega uchumi lililojengwa na TASAF wakiwa mbele ya jengo hilo.
0 Comments