Naibu Waziri wa
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (Aliyesimama katikati
kwenye Chuma) akizungumza katika eneo la ujenzi wa mnara wa TTCL katika kijiji cha
Masenge Mamiwa Wilaya ya Gairo Morogoro wengine ni watendaji aliombatana nao na
wananchi wa eneo hilo.
Naibu Waziri wa
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa kwanza kulia) akizungumza
katika eneo la ujenzi wa mnara wa TTCL katika kijiji cha Masenge Mamiwa Wilaya ya
Gairo Morogoro wakati wa Ziara yake ya kukagua miundombinu na upatikanaji wa
huduma ya mawasiliano katika Mkoa huo.
Naibu Waziri wa Mawasiliano
na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa pili kulia mstari wa mbele) akizungumza
wakati wa ziara yake katika mnara wa mawasiliano wa TTCL uliopo katika Kijiji cha
Kiganira Morogoro vijijini. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya
MorogoroVijijini Mhe. Albert Msando
*********************************
Na Mwandishi wetu, MOROGORO
Shirika la Mawasiliano Tanzania
(TTCL) limetakiwa kuonesha ushindani katika soko la mawasiliano nchini kwa
kupanua wigo wa mtandao wake pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma zake za
laini za simu, vocha, T- Pesa katika maeneo ya mijini na vijijini ili
kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu na ya msingi ya mawasiliano ya
sauti na data
Akiwa katika ziara ya
kukagua miundombinu ya mawasiliano na hali ya upatikanaji wa huduma ya
mawasiliano katika Mkoa wa Morogoro Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia
ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa katika ziara alizofanya Mikoa
ya Mtwara, Kilimanjaro na Tanga amekutana na changamoto za upatikanaji wa huduma
za Shirika hilo wakati wananchi wanahitaji kutumia mtandao wa TTCL
Amesema kuwa tabia za
wateja zinaenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia kwa mfano matumizi ya data kuongezeka kwasababu
ya mitandao ya kijamii na programu tumizi zinazotoa huduma za kijamii hivyo
katika zama hizi za kidijitali Shirika la TTCL linatakiwa kwenda sambamba na
mabadiliko ya tabia za wateja ili kuakisi mahitaji yao
“Shirika la TTCL
mnatakiwa kuboresha na kuongeza wigo wa upatikanaji wa mtandao wenu na huduma
zake badala ya kuweka uwekezaji mkubwa kwenye promosheni halafu wateja wakija
hawapati huduma wanazostahili kuzipata”,
alizungumza Mhandisi Kundo
Aliongeza kuwa ni kazi
kubwa kumrejesha mteja ambaye Shirika litampoteza kutokana na kukosekana kwa
huduma alizotarajia kuzipata hivyo kulitaka Shirika hilo kuboresha miundombinu
yake ili huduma zake ziwe na uwezo unaokidhi mahitaji
“TTCL kuna Minara
imejengwa na imekamilika lakini haijawashwa nendeni mkaiwashe, na ile ambayo
ilikuwa tayari ipo kwenye mpango wa kujengwa ijengwe, inayotakiwa kuongezewa
uwezo iongezewe, kwasababu hili ni Shirika la umma hivyo mnatakiwa kuwafikia
wananchi katika maeneo yote hadi yale yasiyokuwa na mvuto wa biashara”,
alizungumza Mhandisi Kundo
Aidha, amezungumzia huduma ya intaneti yenye kasi kuwa ni huduma
ya msingi yenye mchango mkubwa wa kuipeleka nchi kwenye uchumi wa kidijitali na
kufanyika kwa biashara mtandao ambapo ni wajibu wa Serikali kupitia taasisi za
mawasiliano kuhakikisha wananchi wake katika maeneo yote wanapata na kutumia huduma
ya intaneti
Kwa upande wa wananchi
waliojitokeza katika miradi ya minara ya mawasiliano ya TTCL iliyopitiwa wakati
wa ziara ya Naibu Waziri huyo wamesema kuwa wao wanahitaji kurudi nyumbani kwa
sababu wanaambiwa kumenoga kama kauli mbiu ya Shirika hilo inavyosema “Rudi Nyumbani
Kumenoga” hivyo wameomba kuboreshewa uwezo na ubora wa mtandao huo pamoja
na huduma za vocha, laini za simu na T-Pesa kwasababu katika maeneo mengi
hazipatikani na wakati mwingine wanatembea umbali mrefu kutafuta huduma hizo
Katika ziara hiyo Naibu
Waziri aliambatana na watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ikiwemo
watendaji kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ambapo walipokea
maelekezo ya Naibu Waziri kuhusu kufuata utaratibu wa ujenzi wa miundombinu ya
mawasiliano katika vipengele vya ubora, uwezo, vibali vya ujenzi, mikataba ya
ujenzi na ulinzi na mahitaji ya wananchi kwa ujumla wake na kuahidi kuwa Shirika
litafanyia kazi maelekezo hayo kwa muda muafaka
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara
ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
0 Comments