Ticker

6/recent/ticker-posts

TATHIMINI YA KAMPENI ZA CHAMA CHA MAPINDUZI UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA KONDE PEMBA NA KATA SITA TANZANIA BARA

 Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) Juni 03, 2021 ilitangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo katika jimbo la Konde kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Khatib Said Haji na Udiwani katika Kata sita za Tanzania Bara utakaofanyika kesho Julai 18, 2021. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinashiriki katika uchaguzi huu mdogo kwa ukamilifu.

Kwa mujibu wa ratiba CCM ilifanya uzinduzi wa kampeni zake za Ubunge jimbo la Konde, wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba vivyo hivyo kwenye kata zote sita ambazo ni Mbagala Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Kata ya Ndirigishi iliyopo wilaya ya Kiteto mkoa wa Manyara, Kata ya Mitesa iliyopo Wilaya ya Masasi mkoa wa Mtwara, Kata ya Gare iliyopo Wilaya ya Lushoto mkoa wa Tanga, Kata ya Mchemo iliyopo Wilaya ya Newala mkoa wa Mtwara na Kata ya Chona iliyopo Wilaya ya Ushetu mkoa wa Shinyanga.

CCM inawashukuru sana wanachama, viongozi na wananchi katika maeneo yote hayo kwa namna walivyojitoa na kushiriki kampeni za wagombea wa CCM kwa hamasa kubwa, amani na utulivu.

Aidha kwa tathmini ya kitaalamu CCM inatarajia kufanya vyema katika chaguzi zitakazofanyika Jumapili 18 Juni 2021 katika maeneo ambayo imesimamisha wagombea kwa vile wote wagombea wake wana sifa za uongozi, wanaofahamu mahitaji ya wananchi wao, wanaokubalika na wapigakura zaidi chama kimefanya kampeni za kisayansi sana zilizowafikia wapigakura wengi na makundi yote muhimu kuliko chama chochote na wagombea wa CCM walipokelewa vyema kwa hamasa na matumaini makubwa.

Aidha katika kata sita ambazo uchaguzi utafanyika kesho, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilishatangaza kata nne ambazo CCM imepita bila kupingwa (Chona, Gare, Ndirigishi na Mitesa).Huku kata mbili tu ndizo zitafanya uchaguzi siku ya kesho ambazo CCM imesimamisha wagombea.

Chama Cha Mapinduzi kinatoa wito kwa wanachama wake na wananchi kwa ujumla wa maeneo ya Jimbo la Konde, Kata ya Mbagala Kuu na Mchemo kujitokeza kwa wingi siku ya kesho kuwachagua wagombea wanaotokana na CCM, baada ya kupiga kura warejee majumbani na katika shughuli zao kusubiri matokeo ya uchaguzi.

Chama Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan kinawakikishia kitaendeleza nia na dhamira yake ya kulinda Demokrasia chini kwa vitendo hivyo kitakuwa tayari kupokea matokeo yoyote katika chaguzi hizi zitakazofanyika Juni 18, 2021.

Ikumbukwe kuwa CCM ilifanya hivyo katika uchaguzi wa Uwakilishi wa Jimbo la Pandani uliofanyika 28 Machi 2021 ambapo Chama Cha Act Wazalendo kilishinda uchaguzi huo mdogo kisiwani Pemba.


Shaka Hamdu Shaka
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi
Julai 17, 2021.



Post a Comment

0 Comments