Ticker

6/recent/ticker-posts

TAKUKURU YATOA ELIMU KWA MIKUTANO 27 MANYARA

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari Mjini Babati.

***************************

Na Mwandishi wetu, Babati

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara, imetoa elimu kwa umma kwa makundi tofauti ili kuelimisha jamii katika mapambano dhidi ya rushwa.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati juu ya shughuli zilizofanyika kipindi cha miezi mitatu ya Aprili hadi Juni mwaka huu, amesema makundi mbalimbali yamepatiwa elimu ya kupambana na rushwa.

Makungu amesema jumla ya mikutano 23 imefanyika ikiwa na madhumuni ya kuelezea wananchi kuhusu athari za rushwa na jinsi ya kushiriki katika kupambana nayo.

Amesema katika kutoa elimu ya mapambano ya rushwa, semina saba ziliendeshwa kwa makundi tofauti ikiwemo tatu walizoshirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Sikika.

Amesema katika kipindi hicho cha miezi mitatu, uendeshaji mashtaka na uchunguzi, kesi nane zilitolewa hukumu ambapo kati ya hizo Jamhuri ilishinda kesi sita na mbili watuhumiwa waliachiwa huru.

“Jumla ya kesi mpya nane zimefunguliwa Mahakamani na hadi hivi sasa kesi 40 zinaendelea katika mahakama za mkoa wa Manyara,” amesema Makungu.

Amesema mikakati ya TAKUKURU katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2021, ni kuendeleza na kutekeleza majukumu yao ambapo kipaumbele kitawekwa kwenye uchunguzi wa ujenzi wa nyumba ya mkuu wa wilaya ya Kiteto ambapo mwenge wa uhuru-2021 ulibaini mapungufu kadhaa.

“Tutajielekeza pia katika uchunguzi wa fedha wanazochangishwa wananchi hapa mkoani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambazo zinalalamikiwa kutotumika kwa matumizi yaliyokusudiwa,” amesema Makungu.

Amesema wataendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya mkoa na kudhibiti fedha katika ukusanyaji wa mapato ndani ya halmashauri zote za mkoa wa Manyara.

Post a Comment

0 Comments