Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bw. Donasian Kessy akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa ripoti ya utekelezaji katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2021.
********************************
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imefanikiwa kupokea taarifa 63 kuhusu rushwa pamoja kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi yenye thamani ya shilingi milioni 180.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa ripoti ya utekelezaji katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni mwaka huu, Mkuu wa Taasisi ya TAKUKURU Mkoa wa Temeke Bw. Donasian Kessy, amesema kuwa wamepokea taarifa 107 kati ya hizo 63 ni malalamiko yaliyohusu rushwa.
Bw. Kessy amesema kuwa miongoni mwa taasisi zilizolalamikiwa ni Idara ya Uhamiaji, TANESCO, Mahakama pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Kigamboni katika idara ya elimu, Watendaji wa Kata, Ardhi, afya, utumishi, ujenzi, mazingira pamoja na fedha.
"Uchunguzi wa taarifa hizo unaendelea katika hatua mbalimbali na zile ambazo hazikuhusu rushwa watoa taarifa wameshauriwa hatua ya kuchukua ili kutatua kero zao" amesema Bw. Kessy.
Pia wamefanikiwa kufungua kesi mpya moja, uku mashauri 19 yakiendelea mahakamani pamoja na kuendelea kuelimisha umma juu ya madhara na jinsi ya kupambana na adui rushwa.
"Tumeweza kuelimisha makundi mbalimbali kwa njia ya semina, vyombo vya habari, mikutano ya hadhara, maonesho pamoja na uimarishaji wa klabu za wapinga rushwa" amesema Bw. Kessy.
Bw. Kessy ameeleza kuwa katika kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma walitoa huduma kupitia mpango wa TAKUKURU inayotembea ambapo wananchi pamoja watumishi umma na sekta binafsi kutoka sehemu mbalimbali walipata elimu kuhusu rushwa.
Amebainisha kuwa katika kipindi cha miezi mitatu cha Juluia hadi Septemba, 2021 wataendelea na majukumu ya kuelimisha umma, kuchunguza, kufanya utafiti na udhibiti pamoja na kufatilia utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo.
"Ili kufanikisha mikakati, tuhahakikisha utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo katika Manispaa ya Temeke inafatiliwa kikamilifu katika hatua zote kwa lengo la kubaini iwapo kuna mianya ya rushwa ili kuizibwa kabla ya upotevu wa fedha za serikali" amesema Bw. Kessy.
Bw. Kessy ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
0 Comments