Ticker

6/recent/ticker-posts

SIMBACHAWENE: TUTADHIBITI VIPENYO VYA KUPITISHA MAGENDO MIPAKANI, TUONGEZE MAPATO SERIKALINI

         

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto), akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Siha, Thomas Apson, baada ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Sanya Juu, kilichojengwa na Wadau mbailmbali Wilayani humo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

 

Na Felix Mwagara, MOHA, Moshi.

 

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema serikali itavidhibiti vipenyo zaidi ya 300 vilivyopo katika Mpaka wa Tanzania na Kenya, katika maeneo ya Holili na Tarakea Wilayani Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro.

 

Amasema uwepo wa vipenyo hivyo kumesababisha Serikali kupoteza mapato mengi kwasababu wanaopitisha magendo utumia njia hizo zisizo halali kupitisha bidhaa mbalimbali kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

 

Waziri Simbachawene ameyazungumza hayo jana, katika kikao na Maafisa wa Taasisi mbalimbali wanaofanya kazi katika mipaka hiyo, baada ya kumaliza kukagua na kusikiliza taarifa zao kutoka kwa Taasisi zote katika mipaka hiyo.

 

“Hili jambo halikubaliki, lazima lifanyiwe kazi, nimelipokea ila naomba mjue kuwa kati ya mambo ya msingi kama nchi ni kudhibiti mipaka, huwezi kuwa na nchi alafu watu wanaingia na kutoka wanavyotaka, haiwezekani, lazima nikae na Mawaziei wenzangu pamoja na Makatibu Wakuu tuone jambo hili tunalidhibiti vipi,” alisema Simbachawene.

 

Aliongeza kuwa uwepo wa vipenyo zaidi ya 300, ni vingi sana ila lazima vidhibitiwe kwa kuharibiwa kwasababu Serikali inapoteza mapato mengi na kamwe jambo hilo halitapuuzwa.

 

 

“Suala hili ni la msingi katika maendeleo ya nchi, hivyo siwezi fanya maamuzi peke yangu, naomba niseme kuwa hii taarifa nimeipokea, na nitaipeleka kwa viongozi ili tuone tunafanyaje katika kudhibiti hivi vipenyo, ili watu wapite katika njia halali na zinazoeleweka na kwa hatua hiyo Serikali iweze kupata mapato,” alisema Simbachawene.

 

Kwa upande wake, Mfawidhi wa Uhamiaji Kituo cha Holili, Eliaichi Marandu, alimwambia Waziri Simbachawene kuwa, Mpaka huo unakabiliwa na changamoto ya uwepo wa vipenyo vingi visivyo rasmi hali ambayo inawafanya kushindwa kudhibiti suala la magendo mpakani licha ya kuwa wanajitahidi mara kwa mara kufanya doria.

 

“Mheshimiwa Waziri, vipenyo hivi ambavyo vipo katika maeneo mbalimbali, yakiwemo ya Kamwanga, Rongai hadi mpaka wa Holili, vipo zaidi ya 300 na ni vikubwa hata magari makubwa  yanaweza kupishana, hivyo kuwepo na vipenyo hivi kuna kuwa vigumu kudhibiti licha ya kuwa tunajitahidi kufanya doria,"alisema Eliaichi.

 

Hata hivyo, licha ya changamoto katika mipaka hiyo, lakini kwa upande wa Mpaka wa Tarakea wamevuka kiwango cha ukusanyaji wa mapato ambapo kuanzia mwezi Julai mwaka 2020,

kituo cha Tarakea kilitarajiwa kukusanya shilingi bilioni 13 lakini ilipofika mwezu Juni mwaka huu 2021, kituo hicho kilikusanya  zaidi ya shilingi bilioni 15.

 

Waziri Simbachawene amemaliza ziara yake ya siku mbili Mkoani Kilimanjaro, na Jumatatu Julai 26, 2021 anatarajia kuanza ziara ya Mkoani Arusha ya kukagua utendaji kazi wa Taasisi zake pamoja na miradi mbalimbali.



  Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (wapili kulia) akionyeshwa Mpaka wa Tanzania na Kenya na Mfawidhi wa Kituo cha Holili, Michael Mtoba, wakati alipotembelea Mpaka huo, Mkoani Kilimanjaro, jana. Amesema Serikali itavidhibiti vipenyo zaidi ya 300 vilivyopo katika Mpaka wa Holili na Tarakea. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akizungumza na maafisa wa Taasisi mbalimbali wanaofanya kazi katika Mpaka wa Holili, Mkoani Kilimanjaro, baada ya kumaliza ziara yake, jana. Amesema Serikali itavidhibiti vipenyo zaidi ya 300 vilivyopo katika Mpaka wa Holili na Tarakea. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto), akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Siha, Thomas Apson, baada ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Sanya Juu, kilichojengwa na Wadau mbailmbali Wilayani humo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Waziri George Simbachawene, akipima Virusi vya Corona (COVID 19), katika Mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Tarakea, Wilaya ya Rombo, Mkoani humo, Julai 24, 2021. Majibu ya kipimo hicho yameonyesha hana virusi hivyo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Waziri George Simbachawene, akiangalia wahudumu wa afya katika Mpaka wa Tarakea Mkoani Kilimanjaro, wakijiandaa kumpima Virusi vya Corona (COVID 19), katika Mpaka huo, alipofanya ziara, Julai 24, 2021. Majibu ya kipimo hicho yameonyesha hana virusi hivyo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Post a Comment

0 Comments