NA JUMA ISSIHAKA
SERIKALI imepokea awamu ya kwanza ya dozi za chanjo ya
covid-19 aina ya Johnson & Johnson 1,058,400 kutoka serikali ya Marekani na
kueleza kuwa imefuata miongozo yote na kujiridhisha na usalama wake kwa
matumizi ya binadamu.
Imesema chanjo hiyo itaanza kutolewa baada ya kukamilika
kwa taratibu za ndani za serikali huku yakizingatiwa makundi maalumu wakiwemo
wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 50.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Doroth Gwajima, katika hafla ya kupokea
msaada wa chanjo hizo, iliyofanyika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere
(JNIA) jijini Dar es Salaam.
Amesema kuingia kwa chanjo hiyo, kumezingatia miongozo
yote iliyowekwa na serikali na kwamba huo ni mwanzo wa chanjo nyingi
zinazotarajiwa kuingia nchini.
Kwa mujibu wa Dk. Gwajima, serikali kupitia tume
iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imejiridhisha na kuruhusu kupokelewa
kwa chanjo hiyo.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima |
"Chanjo hii ni salama na imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), Kamati iliyoundwa na Rais Samia na serikali tutaendelea kujirithisha kwa kila chanjo itakayoingia nchini," amesema.
Ameeleza kuwa chanjo hiyo itatolewa katika vituo vya
kutolea huduma za afya na baadhi ya vituo vitakavyoanzishwa ili kusogeza huduma
karibu kwa wananchi.
Amebainisha baada ya kukamilika kwa utaratibu ndani ya
serikali, wataanza kutoa kwa wananchi kwa kuzingatia muongozo, ambapo makundi
maalumu ndiyo yatakayopewa kipaumbele.
“Tumepanga baada ya kukamilika kwa utaratibu wa ndani wa
serikali tutaanza kuitoa bure na kwa hiari na hii tutazingatia muongozo wa
kipaumbele kwa makundi maalumu ambayo ni wahudumu wa afya, wazee wa zaidi ya
miaka 50 na wenye magonjwa nyemelezi,” ameeleza.
Aidha, amesema ujio wa chanjo hiyo isiwe sababu ya wananchi
kuacha kuendelea kuchukua afua nyingine za kujikinga na janga hilo.
“Chanjo zina historia ya kupingwa na baadaye
zinakimbiliwa, mara nyingi zimekuwa zikikabiliana na magonjwa kabla hata ya
dawa kupatikana, mtakumbuka namna chanjo zilimaliza magonjwa kama Surua,
Pepopunda na mengineyo,” amefafanua.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Balozi Libelatha Mulamula, amesema wizara yake itaendelea kushirikiana
na wabia kupata chanjo za kukabiliana na janga hilo na kwamba Tanzania haiwezi
kuishi kama kujitenga.
Amebainisha kuwa chanjo ndiyo njia sahihi ya kujenga
kinga kwa binadamu na kwamba hatua iliyofikiwa sasa ni matunda ya jitihada za
serikali.
“Mimi nimesimama hapa pia muhanga wa janga hili, familia
yangu inasumbuliwa na covid-19 kwa hiyo ugonjwa huu upo, muhimu tujikinge,”
amesema.
![]() |
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dk. Donald Wright, akizungumza wakati wa hafla ya upokeaji chanjo |
Naye, Balozi wa Marekani nchini, Dk. Donald Wright,
amesema msaada huo wa dozi milioni moja ya chanjo ya Covid-19 aina ya Johnson
& Johnson ni sehemu ya jitihada za kimataifa kukabiliana na janga hilo.
Amesema chanjo hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa serikali
ya Marekani ya kutoa dozi milioni 25 kwa nchi za Afrika kati ya dozi milioni 80
zilizoahidiwa kwa Bara hilo.
Kwa mujibu wa Dk. Wright, uratibu wa shughuli hiyo
unahusisha Umoja wa Afrika (AU) na Kituo cha Kudhibiti Maradhi (Africa CDC).
"Tunachangia chanjo hizi ili kuokoa maisha na
kuiongoza dunia katika kulitokomeza janga hilo, pia mchango wetu huu ni
kielelezo cha uimara wa ushirikiano wetu wa miaka 60 na dhamira yetu ya dhati
kwa Tanzania," amesisitiza.
Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani, Dk. Tigest
Katsela, amesema kwa sasa dunia ina visa zaidi ya milioni 191, huku Afrika
ikiwa na visa milioni 4.5 na vifo 108,000.
Amesema kutokana na athari hizo ni budi kujenga nguvu za
pamoja katika kukabiliana janga hilo ili kuokoa uchumi wa mataifa mbalimbali
duniani.
0 Comments