Ticker

6/recent/ticker-posts

RC RUKWA AWATAKA WANANCHI WA MKOA HUO KUZINGATIA MAELEKEZO YA SERIKALI KUHUSU UDHIBITI WA UGONJWA WA UVIKO 19

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa  Joseph Mkirikiti amewataka wananchi wa mkoa huo kuzingatia maelekezo ya serikali kuhusu udhibiti wa ugonjwa wa UVIKO 19 kwa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima ikiwemo kuwa tayari kuchanjwa chanjo itakopoanza kutolewa kwenye vituo vya afya.



Ametoa rai hiyo leo  (27.07.2021) mjini Sumbawanga wakati akitoa tamko kuhusu wananchi kijikinga na tahadhari ya ugonjwa wa UVIKO 19 kwenye kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi mkoa wa Rukwa ambapo ameagiza viongozi wa wilaya na dini kutoa elimu ya kujikinga kwa wananchi kila wanapokutana .



"Wananchi katika mkoa wa Rukwa nawasihi kuzingatia maelekezo ya serikali na wataalam kuhusu kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 ikiwemo kuwaelekeza kujiandàa kupata chanjo kwa wale watakaokuwa tayari" alisema Mkirikiti.



Mkuu huyo wa mkoa ameongeza kusema mkoa wake unaendelea na kazi ya kuhamasisha wananchi kujikinga ambapo amewasihi viongozi wa dini na na serikali kufikisha elimu juu ya umuhimu wa chanjo katika kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Kororna.



Katika hatua za kuhakikisha umma unakuwa na taarifa sahihi Mkirikiti  ameviomba vyombo vya habari mkoani Rukwa kutenga muda mchache kwa wataalam wa afya ili waweze kufikisha elimu ya kukabiliana na UVIKO ikiwa ni kampeni maalum ya nchi.



" Naomba vyombo vya habari mkoa wa Rukwa tengeni muda wa kufikisha ujumbe wa kudhibiti UVIKO 19 kwa kutoa dakika chache kila siku wataalam wa afya kuelezea njia za kujikinga na tatizo hili ili elimu ifike kwa wanachi wengi hatua itakayopunguza kasi ya maambukizo", alisema Mkirikiti .



Mkikikiri aliwaondoa hofu wananchi kuwa chanjo itakayotolewa ni salama kwani serikali lengo lake ni kuwalinda watu wake kuhakikisha usalama wa maisha yao unaekuwepo vizazi na vizazi.
Alibainisha hayo na kuongeza kuwa " hakuna serikali inayoweza kuleta chanjo ya kudhuru wananchi wake, hivyo hii itakayotolewa ni salama " alihitimisha Mku huyo wa Mkoa wa Rukwa.



Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu amesema chanjo ya Jansen ( Johnson  & Jonson) ambayo serikali imeleta nchini ni salama kiafya na kuwa wananchi wasiwe na hofu.



Dkt. Kasululu alisema mkoa wa Rukwa unaendelea kujipanga kutoa chanjo za UVIKO 19 kwa makundi ya kipaumbele ikiwemo watumishi wa afya, watu wenye umri mkubwa zaidi ya miaka 50 na wenye matatizo ya magonjwa ya moyo ,kisukari, kifua kikuu ambapo itatolewa kwa hiari na bila malipo.


Kuhusu takwimu za maambukizi  Dkt. Kasululu alisema tangu Januari 2021 jumla ya watu 80 walipokelewa kwenye vituo vya afya mkoani Rukwa ambapo kati yake 16 walibainika kuwa na UVIKO 19.



" Hadi sasa tunao wagonjwa nane (8) kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa ambapo kati yao wagonjwa wanne (4) wapo kwenye uangalizi maaluum," alisisitiza Dkt. Kasululu.
Katika kikao hicho Dkt. Kasululu amewaomba viongozi wa serikali na na wale wa dini kuwaelekeza na kuwafundisha wananchi kwa kuwaambia ukweli kuwa Kinga ni Bora Kuliko Tiba.


Akiongea kwa kwa niaba ya viongozi wa dini Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Tanganyika Ambele  Mwaipopo ,alisema anaishukuru serikali kwa kutoa elimu juu ya usalama na umuhimu wa chanjo ya UVIKO  19 ambapo amesema watakwenda kuifikisha kwa waumini  na wananchi.



"Tumepokea elimu hii ya kudhibiti UVIKO -19 sasa tunakwenda kufundisha ukweli huo kwa waumini wetu ili hofu iondoke juu ya chanjo itakayotolewa na serikali" alisema Askofu Mwaipopo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akizungumza kuhusu utayari wa wananchi wa Rukwa kupokea chanjo ya UVIKO 19 leo alipofungua kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa mjini Sumbawanga.
Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Rukwa wakifuatilia maelekezo ya serikali kuhusu utayari wa kupokea  chanjo ya kupambana  na Virusi vya Korona ikiwemo  elimu ya kudhibiti  maambukizo ya virusi hivyo.

Post a Comment

0 Comments