Zahanati mbili za vijiji vya Fyengeleza na Kankwale zilizoanzishwa ujenzi wake na wananchi na kukwama kwa zaidi ya miaka 17 sasa zimekamilika na zitaanza kutoa huduma kwa wananchi mwezi Octoba mwaka huu baada ya Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kuzikamilisha.
Akiwa
katika ziara ya kukagua miradi katika Manispaa ya Sumbawanga, jana (29.07.2021)
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Joseph Mkirikiti ameipongeza halmashauri ya
Manispaa ya Sumbawanga kwa kazi nzuri ya kukamilisha miradi hiyo ya zahanati
zilizokwama kwa kipindi kirefu.
Taarifa
zilizosomwa katika miradi hiyo ya zahanati kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa zilieza
kuwa Zahanati ya kijiji cha Kankwale ilianza kujengwa miaka kumi na Saba (17)
iliyopita pale wananchi walipoanzisha ujenzi huo mwaka 2004 huku ile ya kijiji
cha Fyengelezya ikichukua miaka minane (8) kukamilika kutokana na sababu nyingi
ikiwemo usimamizi usioridhisha wa miradi na ukosefu wa fedha.
Taarifa
hiyo ilieleza kuwa zahanati ya Kankwale imegharimu kiasi cha shilingi
81,068,000/- kukamilishwa kati ya hizo nguvu za wananchi zinazotokana na
michango ya fedha tasilimu na nguvu zao kiasi cha shilingi milioni 24 na
Manispaa kupitia mapato yake ya ndani imetumia shilingi milioni 10 na kiasi cha
shilingi milioni 50 kimetoka serikali kuu.
Imeelezwa
kuwa Zahanati ya Fyengerezya hadi kukamilika imegharimu kiasi cha shilingi milioni
75 kati ya hizo Manispaa imechangia
kiasi cha shilingi milioni 25 kutoka mapato yake ya ndani na shilingi Milioni
50 zimetolewa na serikali kuu.
Baada
ya kukagua miradi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Joseph Mkirikiti ameeleza
kufurahishwa na ukamilishwaji wa Zahanati hizo zinazotoa jibu la ukosefu wa
huduma kwa wananchi waliosubiri kwa muda mrefu na kuhoji miaka 17 nini
kilikwamisha.
“Ninawapongeza
viongozi wa Manispaa hii kwa jitihada na ubunifu wa kukamilisha majengo
yaliyoanzishwa na wananchi kwa muda mrefu mfano zahanati ya Kankwale ilianza
kujengwa mwaka 2004 huku ile ya Fyengeleza mwaka 2014 leo tunaona uongozi wa
Manispaa wa sasa ukikamilisha kazi hii na kuwa mwezo Octoba huduma zitatolewa,
ninachojiuliza ni swali hili, kwa nini miaka 17 hizi zahanati zilikwama? Ni
ukosefu wa fedha kweli au ni usimamizi?”. alisema Mkirikiti.
Mkirikiti
aliongeza kuwa jitihada za Manispaa hiyo kukamilisha ujenzi wa majengo ambayo
yalijengwa na wananchi lakini hayakukamilika unatoa suluhisho la upungufu wa
miundombinu ikiwemo shule mpya ya msingi Ntendo “B”, maabara za sayansi shule
za sekondari Kalangasa na Ntendo.
“Wito wangu bado tunao mzigo ni mkubwa ndani
ya manispaa yetu na mkoa wetu wa Rukwa ,hivyo tunapaswa kuongeza kasi zaidi ili
kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kuweza kunufaisha wananchi
huku tukizingatia ubora na matumizi sahihi ya fedha za umma”. alisisitiza
Mkirikiti.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alisema
mafanikio yaliyowezesha kukamilishwa kwa miundombinu hiyo ni ushirikiano
waliopata toka kwa wananchi na watumishi wa halmshauri hiyo .
“Siri
ya kukamilisha miradi hii imetokana na ushirikiano wetu ndani ya Manispaa
wakiwemo Madiwani wetu na pia usimamizi wa miradi shirikishi pamoja na uwepo wa
fedha toka Serikalini” alisema Mtalitinya.
Naye
Mwenyekiti wa Kijiji cha Fyengeleza Frolence Masanja aliishukuru Serikali kwa
kukamilisha mradi wa ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho uliokuwa umekwama miaka
mingi.
Masanja
alisema kukamilika kwa zahanati hiyo kutasaidia wananchi hususan akina mama
wajawazito na watoto kupata huduma karibu zaidi na makazi yao tofauti na ilivyo
sasa ikihusisha kusafiri kwenda mjini Sumbawanga.
Mkuu
huyo wa Mkoa ambaye amehamishiwa Rukwa kutoka Mkoa wa Manyara hivi karibuni
alibainisha lengo la Mkoa wake kuwa ni kuhakikisha majengo ya shule na zahanati
yaliyokwama ujenzi wake yanakamilika kabla ya mwezi wa Octoba mwaka huu ili
kuweza kuruhusu utoaji huduma za elimu na afya.
Mwisho
Imeandaliwa
na;
Afisa Habari Mkuu,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
SUMBAWANGA
30.07.2021
0 Comments