Halmashauri za mkoa wa Rukwa zimetakiwa kutumia fedha za serikali kuu na za makusanyo ya ndani kukamilisha miradi ya maendeleo kwa kuzingatia thamani ya fedha huku miradi hiyo ikiwemo ujenzi wa shule, ujenzi wa hospitali na miradi ya maji ikiwa na ubora .
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (27.07.2021) wakati alipofanya ziara ya kikazi kukagua miradi ya maendeleo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ikiwa na lengo la kufuatilia na kutilia mkazo utekelezaji wa kazi za Serikali tangu alipoteuliwa kuongoza mkoa wa Rukwa hivi karibuni.
Mkuu huyo wa Mkoa ameziagiza Halmashauri mkoani Rukwa kutumia fedha zake za makusanyo ya ndani kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilishwa kwa ubora na wakati ili kero za wananchi kukosa madarasa, maji na huduma za afya ikiwemo ukosefu wa madawa.
“Sasa Serikali imepunguza mzigo kwa halmashauri kwa kulipa posho za madiwani hivyo tunategemea kuona fedha iliyokuwa ikilipwa kwao ikitumika kukamilisha miradi ya maendeleo kwenye kata na vijiji “alisema Mkirikiti ambaye awali alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara .
Mkirikiti ambaye amembatana na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba wakiwa kwenye mradi wa ujenzi wa shule mpya ya kata kijiji cha Kalumbaleza walijionea jinsi madarasa sita yakiwa yamekamilika kwa hatua ya renta kwa gharama ya Milioni 11.5 ikiwa ni nguvu za wananchi mradi ulionza mwaka 2019.
Akiongeoa kwenye mradi huo Mkuu wa Mkoa huyo wa Rukwa aliagiza Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kubadili utaratibu na kutumia mfumo wa kukamilisha ujenzi wa shule moja kwa wakati badala ya kwenda na miradi yote .
“Halmashauri wekeni kipaumbele kukamilisha ujenzi wa maboma ya shule zote tano kabla ya Desemba mwaka huu kwa kuanza na shule moja kila mwezi , hivyo Viongozi kazi yenu ni kuhamasisha na kuwatambua wadau wakiwemo wananchi ili wachangie nguvu na rasilimali fedha kukamililisha ujenzi huo” alisema Mkirikiti.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akiwa kwenye Kitongoji cha Kipenzi Kijiji cha Mfinga alikagua mradi wa maji uliogharimu fedha Shilingi Milioni 102 na kubaini tatizo la uharibifu wa mazingira kwenye chanzo cha maji ambayo ni safu za milima .
Mkuu huyo wa Mkoa akiwa kwenye ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa maabara ya shule ya sekondari Kikware Kata ya Mfinga iliyopo Bonde la Ziwa Rukwa alikemea kitendo cha wataalam wa ujenzi wakiwemo wahandisi kuweka gharama kubwa za miradi kwa kigezo cha makadirio ya kitaalam (BOQ) hali inayosababisha majengo ya Serikali kutokamilika kwa wakati.
“Wananchi wetu hawana dhambi tatizo ni wataalam wetu wa halmashauri maabara hizi zinahitaji Milioni 30 lakini hadi sasa BOQ imewezesha maabara ya kemia pekee bado ya Fizikia na Baiojia. BOQ ni tatizo. Wahandishi wa ujenzi fanyeni kazi zenu kwa uhakika na ubora” alisema Mkirikiti.
Christina Mpepo mkazi wa Kitongoji cha Kipenzi Kata ya Mfinga Sumbawanga alisema anaomba Rais Samia Suluhu Hassan achukue hatua kali dhidi ya wanachi wanaoharibu mazingira ikiwemo wanaochoma moto misitu .
Naye Victoria Credo mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya Sekondari Milenia kata ya Mtowisa aliwasilisha changamoto za ukosefu wa maji ,kutokuwepo kwa umeme na tatizo la upungufu wa madarasa kuwa ni kikwazo kwa shule yao yenye wanafunzi zaidi ya 530 kusoma vema.
Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Apolinary Macheta alisema wamejipanga kukamilisha miradi ya ujenzi wa shule nne za sekondari mwaka huu ili kuondoa upungufu wa madarasa pia kuhakikisha miradi ya ujenzi ikiwemo hospitali ya Mtowisa majengo ya wodi tatu yanakamilika kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti kesho anaendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kuongea na wananchi kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.
Mwisho
Imeandaliwa na;
Afisa Habari Mkuu,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,
SUMBAWANGA.
28.07.2021
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (kushoto) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba (kulia) jana wakiwa kwenye eneo inapojengwa moja kati ya shule mpya ya kata ya Kalumbaleza wilaya ya Sumbawanga. Akiwa hapo Mkirikiti ametoa agizo kwa halmashauri kukamilisha ujenzi huo kaba ya ifikapo mwezi Desemba waka huu ili wanafunzi waanze kusoma.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akishuka mlimani kutoka kukagua tenki la maji wakati alipotembelea mradi wa maji Kasekela kitongoji cha Kipenzi Kata ya Mfinga wilaya ya Sumbawanga jana. Akiwa kwenye eneo hilo alitoa agizo la viongozi wa kijiji kudhibiti matukio ya uchomaji moto msitu yanayoendelea .
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (aliyevaa kofia) akisoma barua ya malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Mfinga jana (27.07.2021) mara baada ya kumaliza ziara ya kukagua mradi wa maji wa Kasekela wilaya ya Sumbawanga.
0 Comments