Ticker

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA KUZINDUA CHANJO YA UVIKO 19 KESHOKUTWA

Rais Samia Suluhu Hassan

 NA MWANDISHI WETU

Ikiwa ni siku mbili tangu Tanzania ipokee msaada wa chanjo aina ya Janssen kutoka Marekani, keshokutwa (Julai 28, mwaka huu), Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuizindua ambapo atakuwa wa kwanza kuchanjwa. 

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, chanjo hiyo itazinduliwa Ikulu ya Dar es Salaam saa tatu asubuhi. 

Imebainisha kuwa baada ya uzinduzi huo, Wizara hiyo itaendelea na taratibu nyingine za usambazaji wa chanjo na namna ya kuzisambaza katika vituo vilivyoandaliwa Mikoa mbalimbali. 

"Kufuatia chanjo hizo kupokelewa nchini, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kufanya uzinduzi wa zoezi la uchanjaji," imeeleza taarifa hiyo. 
 
Aidha, imeweka wazi kuwa uzinduzi wa uchanjaji unaweka historia kwa taifa katika kuendeleza mapambano dhidi ya UVIKO-19 ikiwa ni nyongeza mahususi ya
afua nyinginezo za chanjo ikiwemo unawaji mikono kwa maji safi tiririka na
sabuni, uvaaji wa barakoa katika maeneo hatarishi, ufanyaji wa mazoezi na
upataji wa lishe bora na matumizi ya tiba asili zilizosajiliwa na Baraza la Tiba Asili.

Imebainisha kuwa itoaji wa chanjo ni moja ya afua muhimu na inayoaminika duniani kote katika kupambana na maradhi hususani ya kuambukiza ikiwemo ugonjwa
wa UVIKO-19 hivyo watanzania watumie fursa hiyo.

Imesema baada ya uzinduzi huo, serikali inatarajia kuendelea kupokea chanjo
dhidi ya UVIKO-19 ili kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanachanjwa.

Imewataka viongozi wote
kuiga mfano huo wa kuonyesha njia ya kupata chanjo kwa hiari. 

Post a Comment

0 Comments