Leo Julai 28, 2021 Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mwita Waitara amefanya kikao na Menejimenti ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) pamoja na kufanya ziara ya kutembelea Mradi wa nyumba za Makazi za Magomeni Kota ambapo TBA ni Mkandarasi na Mshauri Elekezi.
Akizungumza katika kikao na Menejimenti ya TBA, Mhe. Waitara ameipongeza TBA kwa kazi nzuri inazofanya ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa miradi mbalimbali ambayo inazingatia viwango vyote vya bora pamoja na kutumia wataalam wa ndani. Pia, Mhe. Waitara ameipongeza TBA kwa kujenga majengo ya kisasa akitolea mfano Ujenzi wa mradi wa jengo la makazi lililopo mtaa wa Simeon Jijini Arusha alilotembelea hivi karibuni ambalo likikamilika litatatua changamoto ya makazi kwa watumishi wa umma.
Katika mradi wa Magomeni Kota Mhe. Waitara ametoa pongezi kwa kazi nzuri iliyofanyika katika mradi huo ikiwa ni pamoja ubunifu wa ziada wa Ujenzi wa vizimba kwa ajili ya wafanya biashara wadogo maarufu kama machinga pamoja na maduka ya kisasa (shopping Malls) ambayo yatasaidia kutoa huduma kwa wakazi wanaozunguka eneo hilo. Pia, Mhe. Waitara amesisitiza usimamizi mzuri wa majengo hayo pamoja na kuhakikisha TBA inatoa elimu kwa watakaokuwa wakazi wa nyumba hizo.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro amemshukuru Mhe. Naibu Waziri kwa kutembelea miradi mbalimbali ya TBA na kumuhakikishia kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa katika ziara hizo.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mwita Waitara akizungumza katika kikao alichokaa na Menejimenti ya TBA baada ya kufanya ziara kwenye mradi wa Magomeni Kota leo jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro akizungumza katika kikao cha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mwita Waitara na Menejimenti ya TBA baada ya kufanya ziara kwenye mradi wa Magomeni Kota leo jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mwita Waitara akikagua ujenzi wa mradi wa Magomeni Kota mara baada ya kufanya ziara ya kikazi kwenye mradi huo leo Jijini Dar es Salaam.
0 Comments