Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka wawekezaji nchini kuwekeza kwenye vivutio vya utalii vinavyopatikana katika Wilaya ya Nyasa ili kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi wa eneo hilo.
Amesema hayo leo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua maeneo ya utalii kwa lengo la kuyaboresha katika ufukwe wa Mpela, kijiji cha Kihagara Wilaya ya Nyasa leo.
“Tutaitangaza Nyasa kuhakikisha kwamba wawekezaji wanakuja Nyasa kuwekeza kwenye fukwe zetu” amesema Mhe. Mary Masanja.
Mhe. Mary Masanja amefafanua kuwa vivutio vya utalii vinavopatikana katika Wilaya ya Nyasa ni vya kipekee.
“Nyasa kuna vivutio vya kipekee kama bustani ya mawe, kuna ziwa Nyasa lenye ufukwe mzuri wenye maji safi, kuna mamba wanaoweza kuwasiliana na binadamu na kuna ngoma za asili zinazohamas” Mhe. Masanja amesema.
Ili kukuza utalii huo, Mhe. Masanja amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kupima maeneo yote ya fukwe na kuyatangaza kwa wawekezaji ili yaanze kuingiza mapato kwa Taifa na kufaidisha wananchi wa maeneo hayo.
Aidha, Mhe. Masanja ameelekeza kuanzishwe matamasha mbalimbali yatakayovutia watalii kutembelea eneo hilo.
“Tutengeneze matamasha ambayo yatavutia wageni kutembelea hapa na tutacheza ngoma zetu za asili ili wageni waone kilichopo hapa na tutaweka viingilio ili wageni wakija waache chochote kitakachowafaidisha wenyeji” Mhe. Masanja amesema
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mhe. Kanali Laban Thomas amesema vivutio vinavyopatikana Nyasa havipatikani sehemu yoyote duniani.
Amemshukuru Mhe. Mary Masanja kwa kuhamasisha na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Wilaya ya Nyasa.
“Tunashukuru kwa kuendelea kuhamasisha na kuelimisha watu kuhusu utalii wa Nyasa kwa sababu watu wengi huwa wanaamini utalii ni wa wanyamapori tu” amefafanua Mhe. Thomas.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhe. Eng. Stella Manyaya amesema Nyasa iko tayari kwa ajili ya kutangaza vivutio vyake vya utalii.
Pia, Mhe. Manyanya amemshukuru Mhe. Mary Masanja kwa kutumia muda wake kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika jimbo lake.
Ziara ya kikazi ya Mhe. Mary Masanja Wilayani Nyasa ni mwendelezo wa ziara zake za kikazi za kukagua maeneo yenye vivutio vya utalii na kuangalia namna bora ya kuyaboresha ili yaanze kutumika kuingiza mapato yatokanayo na utalii.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (wa pili kushoto) akizindua rasmi Bustani ya Mawe itakayotumika kwa shughuli za utalii katika eneo ufukwe wa Mpela kijiji cha Kihagara Wilaya ya Nyasa. Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mhe. Kanali Laban Thomas (wa kwanza kushoto), Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhe. Eng. Stella Manyanya (wa kwanza kulia), Muongoza Watalii, Majoka Nfunguru (katikati) na baadhi ya watendaji na watumishi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyasa.
Naibu Waziri wa Maliasii na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akikagua eneo lenye Bustani ya Mawe baada ya kulizindua rasmi kutumika kwa ajili ya shughuli za utalii, katika ufukwe wa Mpela kijiji cha Kihagara Wilaya ya Nyasa.
Naibu Waziri wa Maliasii na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) na Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mhe. Kanali Laban Thomas wakifurahia utalii wa fukwe katika ziwa Nyasa wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua eneo hilo ili kuboresha mazingira yake kwa ajili ya shughuli za utalii, katika eneo ufukwe wa Mpela kijiji cha Kihagara Wilaya ya Nyasa. Wengine ni watendaji na watumishi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Naibu Waziri wa Maliasii na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akipokea zawadi ya samaki kutoka kwa Muongoza Watalii, Martin Ndoma ikiwa ni ishara ya shukrani kwa kuzindua Bustani ya Mawe katika eneo ufukwe wa Mpela kijiji cha Kihagara Wilaya ya Nyasa.
Naibu Waziri wa Maliasii na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akiwahamasisha wananchi kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana Wilaya ya Nyasa wakati wa ziara ya kikazi katika eneo ufukwe wa Mpela kijiji cha Kihagara Wilaya ya Nyasa.
0 Comments