Ticker

6/recent/ticker-posts

MHANDISI MASAUNI AAGIZA MIKOPO NA MADENI YA BENKI YA TIB KUREJESHWA

Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameiagiza Benki ya TIB kuhakikisha madeni na fedha zote za mikopo zaidi ya shilingi bilioni 535.3 zilizokopeshwa kwa wateja wao bila kufuata taratibu pamoja na wadaiwa sugu zinarejeshwa ili zitumike kutoa mikopo kwenye maeneo mengine yenye tija.

Mhandisi Masauni ametoa maagizo hayo jijini Dar es Salaam alipotembelea Benki ya TIB ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Benki hiyo na wafanyakazi, katika mwendelezo wa ziara zake za kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.

“Kwa njia yeyote ile ni lazima fedha za wananchi zirejeshwe hivyo nawaagiza pia kuleta mapendekezo Serikalini ili kuangalia iwapo kuna eneo ambalo Serikali inaweza kuingilia kati kuhakikisha tunaokoa fedha za wananchi zilizowekezwa katika miradi isiyo na tija”, alieleza Mhandisi Masauni.

Alisema kuwa nchi inapoelekea inahitaji kuona Benki ya TIB inashiriki kikamilifu katika ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati ya Taifa kwa kuiwezesha Serikali kukopa katika taasisi za fedha za ndani badala ya kukopa kutoka benki za nje na kuwataka watendaji wa benki hiyo kusimamia ipasavyo Benki ili jambo hilo liwezekane.

Aidha Mhandisi Masauni ameitaka Benki hiyo ihakikishe mikopo yote inayotolewa iwe na tija ili kuepuka mikopo chechefu na kufadhili miradi inayoweza kuisababishia hasara Benki hiyo na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya TIB, Bi. Mary Mashingo, alisema kuwa taasisi hiyo inashauku ya kushiriki katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea nchini na kusaidia katika kutekeleza Sera katika sekta mbalimbali za maendeleo hivyo itashirikiana na Serikali kubuni mbinu za kuzirejesha fedha zilizokopeshwa kabla ya mwaka 2016 na pia kupunguza riba kwa kuwatumia wataalam mbalimbali.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB, Bw. Charles Singili, alisema kuwa Benki yake kwa kushirikiana na Wataalam kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wanafanya jitihada ya kuhakikisha fedha hizo, zikiwemo shilingi bilioni 168 ambazo kesi zake ziko mahakamani na kiasi kingine cha shilingi bilioni 368 zilizoko mikononi mwa wadaiwa sugu zinarejeshwa ili zitumike kutoa mikopo kwa wawekezaji wengine ili kuchochea upatikanaji wa ajira na pia kodi ya Serikali kupitia miradi hiyo.

Vilevile alieleza kuwa namna pekee itakayoongeza wigo wa kodi ni uwepo wa miradi mingi inayozalisha, na kumhakikishia Mhe. Masauni kwamba Benki yake itazifuatilia fedha hizo ili ziboreshe mizania ya mtaji ya Benki hiyo na kuziwekeza katika meneo yatakayosaidia kujibu matatizo ambayo nchi inakabiliana nayo na kuboresha maisha ya wananchi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) akiiagiza Menejimenti ya Benki ya TIB kukusanya madeni na mikopo yote iliyotolewa mwaka 2016 bila kufuata taratibu, alipofanya ziara katika Benki hiyo, jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya TIB, Bi. Mary Mashingo (katikati) akieleza jambo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) (kulia) alipofanya ziara katika Taasisi hiyo, jijini Dar es Salaam, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Charles Singili.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB, Bw. Charles Singili, akieleza kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Benki yake, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) (hayupo pichani) katika Taasisi hiyo, jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) akiongoza Mkutano wa Menejimenti ya Benki ya TIB, alipofanya ziara katika Taasisi hiyo ikiwa ni muendelezo wa kutembelea taasisi zilizochini ya Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) (katikati), Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya TIB, Bi. Mary Mashingo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Charles Singili, wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Menejimenti ya Benki ya TIB, jijini Dar es Salaam.

(Picha na Wizara ya Fedha na Mipango, Dar es Salaam) 

Post a Comment

0 Comments