Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula,akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 27,2021 jijini Dodoma kuhusu kuimarisha mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni za madini nchini.
.....................................................................
Na.Alex Sonna,Dodoma
TUME ya Madini imesema kuwa hadi Julai 26, mwaka huu jumla ya leseni 443, za utafutaji madini zinadaiwa jumla ya Sh. Bilioni 9.31 zitokanazo na malimbikizo ya ada za mwaka tangu zilipotolewa.
Aidha,wamiliki wote wa leseni ndani na nje ya nchi wametakiwa kulipa malimbikizo hayo ndani ya siku 60, kinyume na hapo hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufuta leseni hizo na wahusika kufikishwa mahakamani.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Prof. Idris Kikula amesema hayo leo Julai 27,2021 wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu kuimarisha mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni za madini nchini.
“Ikumbukwe kuwa lengo la serikali siyo kufuta leseni za wawekezaji bali ni kuhakikisha kuwa sheria, kanuni na taratibu zote zilizowekwa na nchi zinafuatwa na kutekelezwa”amesisitiza Prof.Kikula
Pia, amesema kuwa anawaelekeza maafisa madini wote nchini kufuta leseni zote ambazo hazijaendelezwa na ambazo hazijalipiwa ada ya mwaka kwa mujibu wa sheria ya madini Sura 123 baada ya siku 60, kuanzia tarehe ya tangazo hilo.
“Ndugu waandishi wa habari orodha ya leseni zote ambazao hazijaendelezwa na ambazo hazijalipiwa ada ya mwaka zinapatikana kupitia tovuti ya Madini”amesema Prof.Kitila
Vile vile, amesema kuwa Tume hiyo imeendelea kuongeza kasi ya utoaji wa leseni kwa kuimarisha mfumo wa utoaji na usimamaizi wa leseni za madini.
“Kutokana na kasi hiyo Tume ya madini imeendelea kuwa na mwenendo chanya katika utoaji wa leseni za madini ambapo mwaka 2018/2019 zilitolewa jumla ya leseni 5,094, mwaka 2019/2020 zilitolewa leseni 7,214 na mwaka 2020/2021 zilitolewa jumla ya leseni 7,862 takwimu hizi zinathibitisha ukuwaji wa sekta ya Madini nchini”amesema Prof.Kitila
Aidha, amesema kuwa yapo baadhi ya makampuni na watu binafsi walioaminiwa na serikali na kupewa leseni wameshindwa kutekeleza masharti ya leseni kwa mujibu wa sheria ya madini sura ya 123 ikiwa ni pamoja na kulipa ada ya leseni na kuziendeleza.
“Mtakumbuka kuwa Waziri wa Madini Dotto Biteko katika nyakati tofauti ameendelea kuielekeza Tume ya Madini na kuwahamasisha wawekezaji kuhakikisha wanaendeleza maeneo yao na kulipa ada stahiki za leseni zao”amesisitiza
Kadhalika amesema kuwa lengo la Waziri Biteko, ni kuhakikisha kuwa wawekezaji wanapatiwa taarifa za ziada mapema kabla ya hatua za kisheria hazijachukuliwa.
“Nawasihi wawekezaji wote nchini kuhakikisha wanafuata maelekezo ya Waziri na viongozi wengine wa serikali wakati wote”amesisitiza Prof.Kikula
0 Comments