MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe (UWT) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya ‘Yono Auction Mart’ Scolastika Kevela amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuwaongoza watanzania katika chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 huku akiwataka wananchi kumuunga mkono.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mama Kevela alisema hatua hiyo ya Rais Samia Suluhu Hassan imeiidhihirishia Dunia kuwa Tanzania siyo kisiwa na kwamba haiwezi kujitenga katika kupambana na ugonjwa huo uliopoteza maisha ya mamilioni ya watu tangu ulipotangazwa kuingia duniani.
Kauli ya hiyo ya Mwenyekiti huyo wa UWT Mkoa wa Njombe imekuja muda mfupi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua rasmi chanjo ya ugonjwa huo huku akiwa wa kwanza kupata chanjo hiyo na baadae kufuatiwa na viongozi wengine wa kidini, Chama na Serikali, tukio lilifanyika katika Ikulu ya Dar es Salaam na kurushwa na vyombo mbalimbali vya habari.
“Naungana na viongozi wengine wengi wa Taifa hili wakiwemo wa Chama changu cha Mapinduzi(CCM) pamoja na kidini waliojitokeza na kumpa pongezi Mheshimiwa Rais Samia kwa kuungana na mataifa mengine katika kukabiliana na ugonjwa huu, hatua hii itatuondolea wananchi kasi ya maambuziki lakini pia kutuepusha na vifo” alisema Mama Kevela .
Awali akizindua chanjo hiyo RAIS Samia Suluhu Hassan amesema amejiridhisha kuwa chanjo ya virusi vya corona ni salama na kwamba kama isingekuwa hivyo asingekubali kuwaongoza Watanzania kuchanjwa.
Alisema yeye ni mama wa watoto wanne, mke, bibi wa wajukuu kadhaa, Rais na Amiri Jeshi Mkuu, ana makujumu na kuna watu wanamtegemea hivyo asingeweza kufanya jambo la kuhatarisha maisha yake.
“Kama chanjo sio salama nisingekubali kuchanjwa, nimekubali kuchanjwa kwa sababu ni salama,” alisema Rais Samia katika Ikulu ya Magogoni Dar es Salaam jana muda mfupi kabla ya kuongoza viongozi kupata chanjo ya corona aina ya Johnson & Johnson iliyoletwa nchini Julai 24, mwaka huu kutoka nchini Marekani.
Alisema chanjo zilizopo nchini ni kidogo ukilinganisha na idadi ya Watanzania wanaohitaji kuchanjwa kwa hiyari hivyo serikali itahakikisha zinapatikana chanjo za kutosha.
“Wapo wanaozikataa na wapo wanaozikubali, nawaambia chanjo ni salama kama sio salama nisingekubali kuchanjwa, ninachanjwa baada ya kujiridhisha usalama wake,” alisema Rais Samia.
Aliongeza “Hao wanaozikataa huenda familia zao au koo zao haziathiriwa na janga hili. Ila nendeni Moshi, Arusha na Dar es Salaam kwenye zile koo au familia zilizopoteza wapendwa wao watawaambia na kama wangepewa fursa hii ya kuchanja leo (jana), wangekuja hapa kuchanja,”
Alisema Tanzania si kisiwa ina watu na wengine ni raia wa kimataifa hivyo muingiliano uko duniani kote na lazima tahadhari dhidi ya corona na magonjwa mengine ichukuliwe
Mbali na Rais Samia viongozi wengine waliopata chanjo hiyo ni pamoja na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,Yuda Thadeus Ruwa'ichi, Mufti wa Tanzania ,Abubakar Zubeir, Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania(CDF) Venance Mabeyo, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dk Dorothy Gwajima na wengine wengi wakiwemo waandishi wa habari.
Aidha akisisitiza hilo, Mwenyekiti huyo wa UWT Mkoa wa Njombe Scolastika Kevela aliwataka watanzania kuachana na kauli za upotoshaji kutoka kwa baadhi ya watu kuhusiana na chanjo hiyo akidai kuwa hawana nia njema na afya pamoja na maisha ya watanzania huku akisisitiza kuwa ugonjwa wa Corona upo na unaua na kwamba njia pekee ya kukabiliana nao ni kupata chanjo hiyo.
0 Comments