Meneja Msaidizi Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki, Bi. Victoria Msina akizungumza kwenye mkutano wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya BoT leo jijini Dodoma.
*****************************
Kwa muda mrefu, hali ya uchumi wa Tanzania ilikuwa imara na thabiti, kabla ya kuathiriwa na janga la UVIKO-19 kuanzia mwaka 2020. Uchumi ulikua kwa wastani wa asilimia 6.7 katika kipindi cha 2010-2019, na mfumuko wa bei ulikuwa ukipungua hadi kufikia wastani wa asilimia 3.8 mwaka 2019. Mikopo inayotolewa na benki za biashara kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 15, wakati riba za mikopo zilikuwa zikishuka hadi asilimia 17 kutoka zaidi ya asilimia 20.
Janga la UVIKO-19 limeathiri shughuli za kiuchumi, kutokana na nchi zinazofanya biashara na Tanzania kuchukua hatua kudhibiti kuenea kwa UVIKO-19, ikiwemo vizuizi vya kusafiri. Kwa sababu hiyo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kupunguza athari za janga hilo katika shughuli za kiuchumi na kuchochea ukuaji wa uchumi. Pamoja na hatua hizo, kasi ya ukuaji ilipungua hadi kufikia asilimia 4.8 mwaka 2020 kutoka asilimia 7 kwa mwaka uliotangulia. Ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi pia ulipungua, kufikia ukuaji wa kati ya asilimia 2.3 hadi asilimia 9.1. Viwango vya riba kwa mikopo inayotozwa na benki za biashara vimeendelea kuwa juu, kwa wastani wa asilimia 17, licha ya ongezeko la ukwasi na hatua zingine zilizochukuliwa.
Ili kutoa msukumo mkubwa wa kuongeza kasi ya mikopo kwa sekta binafsi na kupunguza riba, na hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi, Benki Kuu ya Tanzania imeamua kutekeleza hatua za kisera zifuatazo, kuanzia tarehe 27 Julai 2021:
- Kupunguza kiwango cha sehemu ya amana za mabenki kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu (Reduction of statutory minimum reserve requirement-SMR). Benki Kuu imetoa unafuu kwa benki za biashara kwa kupunguza kiwango cha kisheria cha amana ambacho benki na taasisi za fedha zinatakiwa kuweka Benki Kuu, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza sera ya fedha. Nafuu hii itatolewa kwa benki itakayotoa mikopo kwa sekta ya kilimo kulingana na kiasi cha mkopo kitakachotolewa. Aidha, benki itakayonufaika itatakiwa kutoa mikopo kwa sekta ya kilimo kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka. Hatua hii inalenga kuongeza mikopo katika sekta ya kilimo,na kupunguza riba katika mikopo itakayotolewa.
- Kulegeza masharti ya usajili wa mawakala wa benki (relaxation of agent banking eligibility criteria). Benki Kuu ya Tanzania imeondoa sharti la uzoefu wa kufanya biashara kwa angalau miezi 18 kwa waombaji wa biashara ya wakala wa benki. Badala yake, waombaji wa biashara ya wakala wa benki watatakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa au Namba ya Kitambulisho cha Taifa. Hatua hii itachangia kuongeza fedha katika mabenki kutokana na ongezeko la amana na kupunguza riba za mikopo.
- Ukomo wa riba kwenye akaunti za makampuni ya watoa huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi (Limitation of interest rate paid on mobile money trust accounts). Benki Kuu imeweka ukomo wa kiwango cha riba kinachotolewa na benki za biashara kwenye akaunti za makampuni yanayotoa huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi. Riba itakayotolewa kwenye akaunti hizi haitazidi riba itolewayo na benki husika katika amana za akiba (savings deposit rate). Hatua hii inalenga kupunguza gharama za upatikanaji wa fedha kwa benki zinazotumika kukopesha, hivyo kuchangia kupunguza riba za mikopo.
- Kuanzishwa kwa mfuko maalum wa kukopesha mabenki na taasisi za fedha ili ziweze kukopesha sekta binafsi. Benki Kuu imeanzisha mfuko maalum wenye thamani ya shilingi trilioni moja ambao utatumika kukopesha mabenki na taasisi za fedha kwa riba ya asilimia 3, ili taasisi hizo ziweze kukopesha sekta binafsi. Benki au taasisi ya fedha itakayofaidika na mfuko huu itatakiwa kukopesha sekta binafsi kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka. Hatua hii itaongeza ukwasi na kupunguza riba za mikopo kwa sekta binafsi.
- Kupunguza kiwango cha mtaji kinachotakiwa kuwekwa na benki za biashara kwa ajili ya kuweza kutoa mikopo (Reduction of risk weight on loans). Benki Kuu imepunguza kiwango cha mtaji kinachotakiwa kuwekwa na benki za biashara kwa ajili ya kuweza kutoa mikopo. Hatua hii itasaidia kutoa fursa kwa benki za biashara kutoa mikopo zaidi kwa sekta binafsi kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Hatua hizi za kisera zimechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Sura. 197 na Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa, Sura ya 437. Benki Kuu itatoa mwongozo wa namna ya utekelezaji wa hatua hizi kwa benki, taasisi za fedha na makampuni yanayotoa huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi. Pamoja na hatua hizi, Benki Kuu inaziagiza benki za biashara na taasisi za fedha kuweka na kutekeleza mikakati ya kupunguza riba za mikopo na kuhamasisha upatikanaji wa amana.
0 Comments