Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Said |
Na JUMA ISSIHAKA
KATIBU Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zena Said, amewataka wahandisi wanawake nchini kujenga hamasa kwa mabinti kuipenda taaluma hiyo, ili kuongeza idadi ya wanataaluma hiyo wanawake Tanzania.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati akifungua Mkutano na Maonyesho ya bidhaa mbalimbali za wahandisi wanawake, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Aliwataka wachache walipo katika taaluma hiyo kuhakikisha wanaacha alama katika kila shughuli wanazofanya ili kuendelea kujenga uaminifu zaidi kwa jamii.
Mhandisi Zena alifafanua kuwa, ni muhimu kwao kujikita katika ujasiriamali na kuambukiza dhana hiyo kwa wahitimu vyuoni, ili waondokane na mtazamo wa kuajiriwa na badala yake wafungue kampuni zao zinazohusu taaluma.
"Mbali na uhandisi mnapaswa kuwa wajasiriamali, ingawa dhana ya kujiajiri bado haitiliwi maanani na jamii, sio mbaya Mhandisi ukajiajiri katika taaluma yako, serikali imeweka mazingira mazuri ya kuwawezesha ikiwemo mikopo ya asilimia 10 katika kila Halmashauri, " alisema.
Aliongeza hatua ya Taasisi ya Uhandisi Tanzania (IET) kuwa na kitengo cha wanawake ni jukwaa muhimu linalotoa fursa kwao, hivyo wanapaswa kulitumia vizuri.
Katibu Mkuu Kiongozi huyo, aliwasisitiza wahandisi hao, kuwa na mashirikiano chanya kwani ndiyo chachu ya maendeleo yao.
Aliwataka kuwa na utaratibu wa kutembelea vyuo mbalimbali kuzungumza na wanafunzi wa kike wanapohitimu uhandisi, kuhusu namna ya kuwa wajasiriamali katika taaluma hiyo.
Alisema ili kuleta matunda ya taaluma hiyo wanapaswa kuhimizana na kushirikiana katika kubuni miradi itakayoleta mabadiliko katika jamii.
Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB), Mhandisi Patrick Barozi, alisema Bodi hiyo imesajili wahandisi 31,729 ambapo wanawake ni 3,544 sawa na asilimia 11.
Alisema idadi hiyo inaonyesha wajibu wa wahandisi wanawake waliopo kujenga hamasa kwa vizazi vipya wapende masomo ya Sayansi.
Alibainisha kati ya Wahandisi hao wahandisi wajenzi ni 6,541 kati yao wanawake ni 435.
Alieleza Bodi hiyo ina mipango madhubuti kuhakikisha wanatoa fursa kwa wahandisi wanawake ikiwemo kuwasajili na kuwapatia mafunzo mbalimbali.
Alifafanua moja ya mipango ya ERB ni kutoa Bima za afya kwa wahanadisi wanawake ikiwa ni sehemu ya kuwathamini na kujenga hamasa kwa wengine.
Naye, Mhandisi Upendo Haule, ambaye ni Mwenyekiti wa Kitengo hicho cha wanawake, alisema wamekuwa na utaratibu wa kutembelea shule mbalimbali kuhamasisha wasichana kusoma Sayansi ili kuongeza idadi ya Wahandisi nchini.
Alisema wanafnavaya hivyo kwa kujua kuwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania unapaswa kuendana na ongezeko la wahandisi ambao wakati wote ndiyo hutumika kubuni miradi inayotatua changamoto za jamii.
Alisema tayari walishakutana na wanafunzi 100 kuzungumza nao kuhusu suala hilo na wameanza kuona matokeo.
0 Comments