Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ikulu - Zanzibar. Uongozi huo unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Liberata Mulamula (Mb), Naibu Waziri, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma Mohammed Rajab katika ziara rasmi ya kujitambulisha kwa Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
********************************
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi amesema kipaumbele cha Serikali yake hususani katika sekta ya mafuta na gesi,Utalii,Uvuvi Biashara na Uwekezaji ni katika Uchumi wa Buluu ambao utamsaidia Mzazibar katika kuimarisha kipato pamoja na kuondoa kodi za kero kwa Wanzazibar.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa juu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulioongozwa na Waziri wa Wizara hiyo Balozi Liberata Mulamula kwa lengo la kujitambulisha na kupokea maelekezo ya kutekeleza vipaumbele vya Serikali ya mapinduzi Zanzibar.
Dkt. Mwinyi ameilekeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutilia mkazo katika uwekezaji wa maeneo ya Uchumi wa Buluu katika mazungumzo na Mashirika ya fedha duniani ikiwemo IMF na Benki ya dunia ikiwa ni pamoja na wawekezaji na wafadhili mbalimbali kwa kuwa Serikali yake ina imani kuwa bahari ikitumiwa vizuri itainufaisha Zanzibar kiuchumi kuliko maeneo mengine.
Pia Dkt. Mwinyi ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwasaidia wafanyabiashara kutoka Zanzibar kuwaunganisha na wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nje ili Zanzibar nayo iweze kusafirisha bidhaa zake za ndani kwenda nje badala ya kupokea bidhaa kutoka mataifa mengine kama ilivyo sasa.
Amezitaja bidhaa kutoka Zanzibar zinazoweza kusafirishwa Nje ya Zanzibar kuwa ni pamoja na karafuu,samaki na nyama ambazo zina soko kubwa nje ya nchi hususani katika nchi za Kiarabu.
Mbali na hilo Dkt. Mwinyi ametaka kupitiwa upya kwa sera ya mambo ya nje ya nchi hususani katika suala Wazanzibar wanaoishi nje maarufu kama Diaspora ikiwemo kupatiwa hadhi maalum itakayowawezesha kushiriki katika uchumi wa nchi ikiwemo kuwekeza,kubadilishana uzoefu wa kitaaluma na masuala mengine ya maendeleo.
Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amesema Wizara imeyapokea maelekezo ya Rais Dkt Hussein na kwamba tayari kuna mkakati na maelekezo maalum kwa Mabalozi wanaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani ili kuhakikisha mahusiano ya Tanzania na Nchi hizo yanakuwa ya manufaa katika uchumi wa pande zote za Jamuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika tukio jingine Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na ujumbe wake wamekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa kwanza wa Rais Mhe. Othman masoud ambaye kwa upande wake ameeleza nia ya Ofisi yake katika kupambana kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na suala la mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa yameathirika kutokana na mabadiliko ya Tabia nchi jambo ambalo linatishia uhai wa Visiwa mbalimbali duniani ikiwemo Zanzibar.
Katika tiara hiyo Balozi Mulamula ameambatana na Naibu Waziri Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk,Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine,Naibu Katibu Mkuu Balozi Fatma Mohammed Rajab pamoja na baadhi ya Wakurugenzi wa Idara na Vitengo via Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
0 Comments